December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabadiliko ya Tabianchi yanachochea ongezeko la Magonjwa

Na Penina Malundo, Timesmajira

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema Dunia kwa sasa inapitia wakati mgumu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanapelekea kuongezeka kwa magonjwa ikiwemo magonjwa ya mlipuko pamoja na majanga yayoathiri Afya za watu.

Waziri wa Afya , Ummy Mwalimu amesema hayo leo Mei 29, 2024 wakati akihutubia kwenye Mkutano wa 77 wa Shirika la Afya Dunia (WHO) unaoendelea kufanyika katika Jiji la Geneva nchini Uswisi.

“Tanzania ni moja kati nchi zilizoathirika na mabadiliko ya tabia nchi ambapo tunaendela kushuhudia ongezeko la joto kali, mvua kubwa inayosababisha mafuriko, maporomoko ya ardhi, ongezeko la magonjwa ambapo vyote hivi vimesababisha madhara kwa Afya za binadamu na kupelekea kusababisha vifo.” Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy akiendelea kuhutubia mkutano huo wa 77 wa Shirika la Afya Dunia(WHO), katika hotuba yake amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Ghebreyesus kwa uongozi wake imara ikiwa Dunia inapitia wakati mgumu wa mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha, Waziri Ummy baada ya kuhutubia Mkutano huo amekutana na Taasisi ya ‘Susan Thompson Buffet Foundatiion (STBF)’ kwenye kikao cha pembezoni kilichoandaliwa na Taasisi hiyo ambapo kwa pamoja wamejadiliana kuhusu kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Katika kikao hicho waziri Ummy amesema, Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupiga hatua katika kutekekeza afua za Afya ya Mama na mtoto ambapo imeweza kupunguza vifo vya wajawazito kutokana na utashi wake wa kisiasa.

Kwa upande wa wadau hao kutoka Taasisi ya ‘Susan Thompson Buffet Foundatiion (STBF)’ wamesisitiza kuwa, wataendelea kufanya kazi na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika eneo hilo muhimu la kupunguza vifo vya Mama wajawazito na watoto.