June 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabadiliko ya Tabianchi chanzo cha kuathiri Lishe Bora

Na Penina Malundo, Timesmajira

MABADILIKO ya hali ya hewa nchini ni miongoni mwa sababu inayochangia kuathiri kwa sekta ya lishe kutokana na mvua zinazonyesha kutoeleweka na wakati mwingine kuwa  nyingi au chache.

Kutoeleka kwa mvua ni chanzo cha kusababisha kasi ya uzalishaji na usambazaji wa mazao kudhorota na kufanya chakula kuuzwa kwa bei ya juu na kuwawafanya watu kutopata lishe kamili.

Watafiti mbalimbali wa masuala ya lishe wamekuwa wakisema kuwa mabadiliko ya tabianchi ni chanzo cha kusababishe lishe kuzorota kwa baadhi ya watu kutokana na kutopata lishe kamili inayotakiwa.

Pia wanasema mabadiliko hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa magonjwa hatarishi kama kipindupindu endapo mvua inapokuwa kubwa na kuzalisha vijidudu vinavyoathiri chakula masokoni kwa kuingiliwa na vimelea vya vijidudu visivyofaa.

Lakini tumekuwa tukishuhudia mara kwa mara Mamlaka ya hali ya hewa nchini,ikitoa tabiri zake katika misimu ya mvua ili jamii,wakulima wadau mbalimbali wa sekta kuhakikisha wana ambapo kwa kiasi kikubwa inasaidia wananchi hususan wakulima kujua wanajipangaje na misimu hiyo.

Kuna umuhimu wadau wa kilimo kwa kushirikiana na wizara husika kutoa ushauri kwa wakulima ili kuweza kulima mazao mchanganyiko yanayoendana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yataweza kukabiliana na hali yoyote ile katika misimu yote ya mvua.

Kwani endapo watu hawatapata chakula cha kutosha kunauwezekano wa hali ya juu kuathiri mifumo yao ya chakula na kusababishwa kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo Utapiamlo.

Afisa Lishe Mtafiti kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mwananyamala,Walbert Mgeni anasema kuna uhusiano mkubwa kati ya hali ya hewa na masuala ya lishe.

Anasema endapo mtu hakikosa chakula  kunauwezekano mkubwa wa yeye kupata utapiamlo ambapo ugonjwa huo unasababishwa na kukosa kwa chakula.

Mgeni anasema kutoana na kipindi cha mvua kuna hali ya hewa ambayo sio rafiki mara nyingi kunakuwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula hususani kwa wakulima hivyo kusababisha chakula kutofika masokoni kwa wakati na bei kuwa ya juu.

Anasema kipindi cha mvua ni muhimu jamii kujipanga kula chakula mchanganyiko ambacho kinachoweza kupatikana msimu wa mvua.

”Mara nyingi hali ya hewa ikiwa mbaya inathiri upatikanaji wa chakula na kufanya bei  ya vyakula kuwa juu hii inatokana na usafiri unakuwa wa shida kwa wachuuzi kutokana na miundombinu ya barabara hali inayofanya watu kukosa mlo kamili,”anasema na kuongeza

”Na kukiwa na baridi ulaji wa chakula  unakuwa tofauti na ule ulaji wa kila siku kwani unakuta kipindi cha baridi mtu anakula sana ambapo kitaalamu inaitwa (Kimetaboriki)hivyo kumfanya kutokosa chakula wakati huo,”anasema.

Anasema ni vema kipindi hicho kuhakikisha jamii inakula mlo mchanganyiko unaopatikana   kutoka makundi mbalimbali ya chakula.

Anasema kwa kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa uimarikaji wa lishe nchini.”Kipindi cha mvua nyingi unakuta vyakula vinapanda bei na kusababisha familia zenye vipato vya chini kushindwa kumudu bei hizo na kusababisha kutokula mlo kamili badala yake wengine wanakula mlo mmoja na wengine kutokula kabisa,”anasema.

Mgeni anasema wakulima wanapaswa kwa sasa kuanza kulima mazao ambayo yanayostahimili hali ya ukame ikiwemo mtama,mihogo pamoja na mahindi ili kuja kusaidia kuwa na jamii yenye afya nzuri inayoendana na lishe kamili.

”Tayari Tanzania ni miongoni mwa nchi tunayopambana kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa hivyo  ni vema kuhakikisha wakulima wetu sasa wanapatiwa elimu ya ulimaji wa mazao ambayo yanakabiliana na mabadiliko hayo,”anasema.

Aidha anasisitiza ni lazima kuimarisha mnyororo mzima wa chakula kuwa mzuri katika misimu yote ya mvua na joto kwani isipokuwa mzuri inaathiri mnyororo wa chakula.

”Mnyororo wa chakula utakapoimarisha kukawepo kwa miundombinu mizuri ya barabara hata kama mvua ikinyesha haiwezi kuathiri upatikanaji wa chakula kwa sababu upatikanaji wa chakula unapoathirika unaathiri bei kupanda katika masoko na kufanya watu wa kawaida kushindia mlo mmoja,”anasisitiza.

Naye Mtafiti Lishe Honest Kombe anasema mara nyingi kipindi cha msimu wa mvua kupanda na kushuka kwa bei za mazao ni jambo ambalo linalotegemewa na watu wengi kutokana na mazao kutoingia sokoni au kuingia kwa kidgo kidogo.

Anasema hali ya mwenendo wa kunyesha kwa mvua za vuli na za  msimu inachangia kwa asilimia kubwa wafanyabiashara wa nafaka nchi kutoingiza zao hilo kwa wakati hivyo kuongeza kasi kwa wananchi na kufanya bei kupanda.

”Kipindi cha mvua kuna hali ya hewa ambayo sio rafiki sana,hivyo suala la lishe linakuwa linachangamoto kubwa  sana hususan katika kwenye uandaaji wa vyakula kutokana na uchafu unaokuwepo mwingi masokoni na mashambani.

”Ni vema kuhakikisha  maandalizi ya chakula yanakuwa masafi katika suala la uandaaji wa chakula hususan kipindi cha mvua nyingi ili kusaidia  kuondoa vimelea vya magonjwa,”anasema.

Akitolea mfano,Kombe anasema unakuta kipindi cha mvua matunda kama maembe yanakuwa mengi na yanapaswa kuoshwa vizuri kwa maji safi tiririka ili kuondoa vimelea vya magonjwa na kusaidia kuondoa magonjwa ya Kuhara na Kipindupindu.

Anasema magonjwa ya Kipindi cha mvua yanalipuka kutokana na hali ya unyevunyevu kuruhusu vimelea vya magonjwa kuingia katika vyakula na kufanya lishe kuwa na changamoto.

”Kipindi cha mvua tunakuwa karibu na jamii kuelimisha namna ya kula lishe iliyozuri kwa kuandaa chakula kwa usafi ili hata mlaji wa chakula hicho kula bila kupata changamoto yoyote,”anasema.

”Anasema pia kipindi hicho kinapaswa kuhakikisha vyakula vinakaushwa vizuri na kutunzwa ipasavyo katika kuhakikisha wadudu wala unyevunyevu kutoingia,”anasisitiza.

Aidha anasema kuna mahusiano kati ya hali ya hewa na lishe kwani endapo mtu anapokosa chakula ni lazima aje apate utapiamlo kwani magonjwa hayo yanasababishwa na ukosefu wa chakula.

”Endapo kuna mvua nyingi au jua kali na  wakulima  hawajalima mazao mengi au hawajalima vizuri lazima wananchi wakose vyakula hivyo kusababisha watu kutopata lishe kwa uhakika na badala yake kuugua magonjwa ya utapiamlo,”anasema.