Joyce Kasiki na Zena Mohamed, TimesMajira Online- Dodoma
RAIS Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuweka utaratibu mzuri ambao hautaleta usumbufu wa uchukuaji wa maiti hospitalini badala ya kuzuia maiti.
Amesema utaratibu wa sasa ambao umekuwa ukiwazuia wananchi kutoa maiti hospitalini kwa kigezo cha kulipa gharama za matibabu kabla ya kifo siyo mzuri.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma wakati wakizungumza na Wanawake wa Tanzania kupitia Wanawake wa mkoa wa Dodoma.
“Natoa maagizo kwa Waziri wa afya kuweka utaratibu mzuri wa ghrama za matibabu wakati wa matibabu yakiendelea ili kuondoa changamoto ya kuzuia maiti kwa kigezo cha kudaiwa gharama hizo,“amesema na kuongeza kuwa,
“Moja ya mpango mzuri ni kutoa gharama za matibabu kabla ya mgonjwa kufariki siyo hadi mgonjwa amefariki ndio umwambie bila kulipa deni lako milioni tatu au ngapi hiyo hapana,tuweke mpango mzuri siyo kuzuia maiti,”amesema.
Changamoto kielimu watoto wa kike
Aidha, Rais Samia alizungumzia kuhusu mafanikio ya elimu bure ambapo alisema pamoja na kuchukuliwa kwa hatua hiyo lakini bado watoto wakike wanakabiliwa na changamoto katika mifumo ya elimu ikiwemo uhaba wa madarasa,mabweni .
“Licha ya kwamba changamoto katika eneo hili zinagusa jinsia zote lakini wanaoathirika zaidi ni watoto wa kike,”amesema
Amesema,Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya elimu ili kuondoa changamoto hizo ambazo zinawahusu jinsia zote mbili lingawa waathirika wakubwa ni watoto wa kike .
Sambamba na hayo amesema, kwa lengo la kuongeza fursa za elimu na kuwafanya wanawake wanufaike na fursa za elimu kwa ujumla ,mwezi Julai mwaka huu Serikali itaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa sekondari yenye mabweni kwenye kila mkoa kwa ajili ya masomo ya sayansi kwa wasichana.“Na kwa sababu waziri wa elimu ni mwanamama sina shaka hili atakwenda nalo vizuri.”
Wasichana waongezeka vyuo vikuu
Kwa mujibu wa Rais Samia idadi ya wasiichana imeongezeka vyuo vikuu kutokana na kuwepo kwa mfuko wa vyuo vikuu huku akisema mfuko huo utaendelea kuongezwa kila mwaka.
Alisema,Takwimu za hivi karibuni ,mwaka 2021 jumla ya shilingi bilioni 464 ziliztengwa huku mwaka ujao wa fedha wa 2021/22 jumla ya shilingi bilioni 500 zinatarajiwa kutolewa kwa ajili ya kuwezesha watoto wavulana na wasichana kuingia vyuo vikuu.
“Kule nyuma ambapo wazazi walikuwa wanalipia ada vyuo vikuu,na wasichana kuachwa tofauti na sasa ambapo huchukuliwa wote kulingana na sifa zao,”amesisitiza
Uwezeshwaji wanawake kiuchumi
Kuhusu uwezeshwaji wanawake kiuchumi alisema tangu uhuru kumekuwepo na Mifuko 61 imeanzishwa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Amesema, tangu kipindi hicho jumla ya shilingi trilion 2.2 na zaidi zimetolewa kwa wanawake ambapo jumla ya wanawake milioni 5.3 wamenufaika.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wanawake wajitathimini kutokana na kupata kiasi hicho cha fedha na nini wamefanya cha kuwaletea maendeleo yao.
“Hapa kuna somo , toka uhuru hadi leo hii kuna la kujifunza ,kwamba pesa yote hii imeingia kwa wanawake ni vyema tujitathimini pesa hizo zimefanya nini ,tuna mafanikio gani yamepatikana kwenye hii,je zote hizi zimeingia kwa mikono ya wanawake ?alihoji Rais Samia.
Mikopo ya Halmashauri
Amesema,mwaka 2018 Serikali ilipitisha sheria ambazo ziliielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo bila riba kwa wanawake 4%, vijana 4% na wenye ulevumavu 2%.
Kwa mujibu wa Rais Samia tangu 2018 mikopo yenye thamani ya Shilingi bil. 63 na milioni 489 imetolewa na kuwanufaisha wanawake 938,802.
Benki ya Posta Tanzania imeendelea kutoa mikopo kupitia dirisha la wanawake, hadi sasa bil 22 na milioni zimetolewa kwa wanawake 6,327.
“Naziagiza mikoa, wilaya na halmashauri kuendelea kuyatunza na kuyasimamia majukwaa yote ya wanawake yanayowawezesha na kutoa mikopo, nasisitiza kwa sababu najipanga kikamilifu kuyalea majukwaa hayo,”amesisitiza
Ukatili kwa wanawake
Amesema, kutokana na changamoto za mila na desturi hapa nchini wanawake wengi hawana uwezo wa kumiliki mali ikiwemo ardhi na nyumba huku akisema taarifa zinaonesha 7.4% ndio wana umiliki wa nyumba ukilinganisha na 25.6% ya wanaume, na umiliki wa ardhi ni asilimia 8.1 ya wanawake huku wanaume wakiwa idadi nzima iliyobaki.
Amesema,hali hii inawakwamisha wanawake kujikwamua kiuchumi huku akiitaka jamii kuachana na dhana hii kwa kuwapatia wanawake haki sawa kama wanaume.
Pia ametumia fursa hiyo kumwagiza Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu kuhusu mikopo ya halmashauri kwenda kusimamia mikopo ya vikundi ili itolewe bila ubaguzi.
Kwa upande wa Serikali amesema,imefanya jitihada kubwa kwenye kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ikiwemo kuanzisha madawati ya jinsia ya wanawake kwenye vituo vya polisi 420, kamati 18, 186 za ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto zimeanzishwa kuanzia ngazi ya kijiji, mtaa hadi Taifa.
“Wanawake tukae tujiangalie tumekwama wapi, tunakosea wapi, kitu gani hakiko sawa ili tuweze kuondokana na unyanyasaji tunaokumbana nao kwenye baadhi ya maeneo,”amesema.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari