November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maafisa usafirishaji/wafanyabiashara Gerezani kuwekewa mazingira mazuri ya shughuli zao

Na Agnes Alcardo, TimesMajira Online, Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema Serikali itahakikisha inaweka mazingira mazuri yatakayo warahisishia Maafisa usafirishaji wa Kariakoo, hususani wa Kata ya Gerezani, ili kuhakikisha wote wanafanya shughuli zao kwa usawa na kutegemeana.

Hayo yamesemwa leo, Machi 9, 2024 Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya hiyo, alipokuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa kusikiliza kero za wananchi, wafanyabiashara na maafisa usafirishaji wa Kata ya Gerezani iliyopo Kariakoo Jijini Dar es Salaam.

Akijibu baadhi ya kero ,zilizotajwa na baadhi ya maafisa usafirishaji na wafanyabiashara, katika mkutano huo, ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azan Zungu, ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mpogolo amesema, kero zote zitatatuliwa kwa kutumia njia ya maridhiano ili kila mmoja ajipatie kipato na kuweza kujikwamua kiuchumi.

Kati ya kero kubwa zilizotajwa katika mkutano huo ni pamoja na muingiliano kati ya madereva ‘kirikuu’ na Tax, ambao wameealalamikia waendesha pikipiki za magurudumu mawili ‘bodaboda’ kuegesha katika maeneo yao na kubeba mizigo kinyume na Sheria ambayo haiwataki kubeba huku ikitolewa mfano, kuwa wamekuwa wakibeba magodoro, mbao na vifaa mbalimbali, hali ambayo inawasababishia madereva ‘kirikuu’ na Tax kushindwa kufanya biashara.

Lakini pia, madereva ‘kirikuu’ wamewalalmikia madereva ‘bajaj’ kutofuata utaratibu wa maegesho ya vyombo vyao vya moto hali inayopelekea kuwepo kwa msongamano barabarani na madereva ‘kirikuu’kushindwa kushusha mizigo kwa wakati madukani.

Mpogolo amesema, zipo changamoto nyingi ambazo Serikali imekuwa ikipokea kutoka kwa watu mbalimbali na kudai kuwa kila changamoto inatatuliwa kulingana na mazingira husika ili kutenda haki kwa kila mmoja na kudai kuwa changamoto zote zitatatuliwa hivi karibuni.

“Sisi tunaishi kwa kutegemeana na ninyi wote hapa ni wafanyabiashara, kuna maafisa usafirishaji, mpo madereva bodaboda hapa, madereva bajaj, madereva tax, waendesha kirikuu na wafanyabiashara wa kwenye fremu bila kuwasahau wakazi wa maeneo haya, sasa kila mmoja akimlalamikia mwenzake kuwa huyu haitajiki atolewe hili halijakaa sawa.

” Kwani wote hapa mnategemeana, wewe mfanyabiashara wa kwenye fremu utamuhitaji bodaboda akukimbizie mzigo haraka sehumu fulani, mfanyabiashara pia utahitaji kirikuu ije ikuletee bidhaa hapo dukani kwako, hivyo hivyo kwa kila mmoja ndiyo maana tunasema wote mnategemeana isipokuwa ipo haja ya sisi kama Serikali ngazi ya Wilaya kukaa na wawakilishi wenu na kuangalia njia ya kuwapanga kila kundi kwa nafasi yake ili kila mmoja ajipatie riziki kwa nafasi yake”, amesema Mpogolo.

Pia ameongeza kuwa, Serikali kwa kuendelea kuonesha inawajali wananchi wa Jimbo la Ilala, kupitia Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo, imeendelea kuleta maendeleo katika Sekta mbalimbali, ambapo kwa upande wa elimu kujenga shule nne zilizo katika mtindo wa ghorofa, shule ya Mchikichini, Lumumba Gerezani na jangwani.

Huku Bilioni 5 zikielekezwa katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mchikichini, kikiwa kituo pekee cha Afya kilichogharimu kiasi kikubwa cha pesa kuliko vituo vyote katika Wilaya ya Ilala, huku Bilioni 4 ikielekezwa Katika ujenzi wa barabara na mitaro.

Nae Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, amewataka wafanyabiashara na Maafisa usafirishaji wa Kariakoo, kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya kufanyia biashara, huku akiwataka na wao kuboresha huduma katika biashara zao, ili kuendelea kuwavutia wateja wao.

” Ni lazima na nyie mtambue kile mnachokifanya, jitahidini kuboresha mazingira yenu ya ufanyaji biashara kwani vipo vitu vingi vinavyoweza mvutia mteja kuja kupata huduma kwako, kama una duka basi weka hata maji kama zawadi ya mteja pindi anapikuwa dukani kwako akipata huduma, kama ni dereva basi uwe na lugha nzuri kwa abiria wako ikiwezekana msaidie kumfunga hata mkanda, hiyo ndiyo njia nzuri katika ushindani wa kibiashara”, amesema Zungu.

Mkutano huo, pia ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa pamoja na Diwaki wa Kata ya Gerezani Fatuma Aboubakar.