November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ma-RC Tabora, Kigoma wapongeza maboresho makubwa TRC

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAKUU wa Mikoa ya Tabora na Kigoma, Balozi Dkt Batilda Burian na Thobias Andengenye wamempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake kubwa ambazo zimewezesha kuboreshwa kwa huduma za usafiri wa reli nchini.

Wakizungumza katika ziara maalumu ya kujionea hali ya miundombinu ya reli kutoka Stesheni ya Tabora kuelekea Mkoani Kigoma, Viongozi hao wamesema serikali ya awamu ya 6 imefanya kazi kubwa kuhakikisha huduma za usafiri wa reli zinaboreshwa kwa kiasi kikubwa tofauti na huko nyuma.Walieleza kuwa Shirika la Reli nchini (TRC) sasa linajivunia kuwa na miundombinu mizuri ambayo sasa inawawezesha kutoa huduma bora za usafiri wa abiria na usafirishaji mizigo kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Wakuu hao wakiambatana na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mikoa na wadau mbalimbali wa maendeleo walisafiri kwa treni kutoka Mkoani Tabora hadi Kigoma ili kujionea raha ya usafiri huo na vivutio vya utalii vilivyopo.

Dkt. Batilda alibainisha lengo la safari hiyo ya kihistoria kuwa ni kuunga mkono kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais na kumshukuru kwa kuwaboreshea wananchi huduma za usafiri huo ili kuharakisha maendeleo yao.

‘Tunamshukuru sana Rais kwa kuiwezesha TRC kupata mabehewa mazuri ambayo yamefanya usafiri wa reli kutoka Dar es Salaam kuja Tabora hadi Kigoma sasa kuwa bora zaidi na kuchochea shughuli za maendeleo ya wananchi’, alisema.

Aidha Dkt.Batilda aliongeza kuwa mpango wa serikali ya awamu ya 6 wa kujenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Dodoma hadi Kigoma ni mkombozi kwa wakazi wa Mikoa hiyo kwani utapunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kusafiri kutoka Dodoma kuja Tabora na Kigoma.

Aliwataka wakazi wa Mikoa hiyo kutunza mabehewa hayo kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vya baadae kwani kutokufanya hivyo ni kupinga jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassani.

Aidha aliomba uongozi wa TRC kusimamia vema huduma wanazotoa na kutunza vizuri mabehewa hayo kwa kuwa yamegharimu fedha nyingi za serikali.

Wakiwa ndani ya treni hiyo viongozi hao walipata fursa ya kuongea na wananchi na kutoa zawadi kwa baadhi ya abiria walioungana nao katika safari hiyo.

RC Andengenye wa Kigoma alisema hatua ya Rais Dkt. Samia kuongeza mabehewa kutoka 7 hadi 22 ametatua kero ya muda mrefu ya wakazi wa Mkoa huo hasa wanaoishi vijijini kwani wengi wao hutumia usafiri huo ikiwemo kusafirisha mazao na bidhaa nyinginezo.

Aliongeza kuwa maboresho hayo yamewezesha usafiri huo kuwa mara 4 kwa wiki tofauti na huko nyumba ambapo treni ilisafiri mara mbili (2) tu kwa wiki, na kubainisha kuwa maboresha hayo yatachochea maendeleo katika sekta ya kilimo, viwanda na biashara kwa Tanzania na nchi Jirani za Kongo, Burundi na Rwanda.

Aliungana na Balozi Dkt Batilda kuwataka wakazi wa Mkoa huo kutunza na kulinda mabehewa hayo ili yawe na tija kwa maendeleo ya taifa.

Mbali na maboresho hayo Andengenye alibainisha kuwa serikali pia imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha usafiri wa majini katika ziwa Tanganyika ambao umekuwa changamoto kubwa kwa wakazi wa Mkoa huo na kuongeza kuwa kazi ya ujenzi ya barabara ya lami inayounganisha Mikoa hiyo pia inaendelea kwa kasi kubwa.

Mwenyekiti wa CCM MKoani Tabora Hassan Wakasuvi alipongeza kuboreshwa kwa usafiri wa treni katika Mikoa hiyo kwani ni usafiri unaotumiwa na wananchi wengi kutokana na unafuu wa nauli.

Aliomba Shirika hilo kuongeza usimamizi wa miundombinu hiyo ili kuepusha uhujumu wa reli na mabehewa hayo ili yadumu tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wa Mkoa wa Tabora, Mohamed Nassoro Hamdan alimpongeza Rais Samia kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa kasi kubwa katika sekta zote ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Wakuu wa Mikoa ya Tabora na Kigoma, Balozi Dkt Batilda Burian wa Tabora (wa tatu kutoka kushoto mstari wa mbele) na Thobias Andengenye wa Kigoma (wa nne kutoka kushoto mbele) wakiwa na Viongozi mbalimbali wa CCM na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa hiyo wakati wa ziara maalumu ya kihistoria ya kusafiri na treni ya kati kutoka Tabora kwenda Kigoma ili kujonea maboresha makubwa ya usafiri huo yaliyofanywa na Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan.( Picha na Allan Vicent.)