November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lukuvi avipatia vijiji vitatu ardhi ekari 300

Na Munir Shemweta,TimesMajira Online,Same

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameshusha neema kwa vijiji vitatu vya Ndungu, Msufini na Mperani vilivyopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro kwa kuvipatia ekari mia tatu kila kijiji kwa ajili ya makazi na kuagiza kufanyika ukaguzi wa mashamba makubwa nchini kubaini yasiyoendelezwa.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akifurahiwa na wananchi wa Tarafa ya Ndungu wilayani Same baada ya kuwatangazia kupata ekari 300 katika vijiji vya Msufini, Mpirani na Ndungu

Hatua hiyo inafuatia wananchi wa vijiji hivyo kuomba kupatiwa sehemu ya ardhi ya Mwekezaji Kampuni ya LM Investment kwa ajili ya makazi ambapo baada ya uamuzi sasa Mwekezaji atabakia na jumla ya ekari 2,452.844.

Akizungumza na wananchi wa Ndungu wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro jana, Lukuvi amesema baada ya mwekezaji kuachiwa ekari hizo 2,452.844 anachotaka ni kuona uwekezaji wa uhakika unafanyika na kusisitiza asipofanya uwekezaji atanyang’anywa shamba.

Amemuonya Mwekezaji kwa kumtaka kuhakikisha shamba lake linapandwa mkonge na kusisitiza ardhi hiyo lazima itumike ili vijana waajiriwe na kubainisha kuwa haiwezekani mwekezaji kuwa na ekari 2,452.844 halafu atoe ajira ya watu 50 tu.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi skioneshwa ramani na wataalam wa sekta ya ardhi katika eneo la Shamba la Ndungu wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kabla ya kutangaza kulimega shamba hilo na kuvipatia ekari 300 vijiji vya Msufini, Mpirani na Ndungu

“Hatufukuzi wawekezaji bali tunataka maendelezo katika shamba na tunataka muwekezaji kuacha kutumia mkopo kuendeleza maeneo mengine,” amesema Lukuvi.

Wananchi wa vijiji hivyo vitatu waliomba kupunguziwa ardhi kutoka kwa Mwekezaji kwa maelezo ya kutokuwa na ardhi ya kutosha kwa ajili ya makazi kutokana na ardhi yao kuwa tepetepe.

Ombi la wananchi hao, lilisababisha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuona umuhimu wa wananchi hao kupatiwa ardhi kwa ajili ya makazi na kupunguza sehemu ya shamba la Mwekezaji na kukipatia kila kijiji ekari mia moja.

Tayari taratibu zote za upimaji na upangaji eneo hilo zimefanyika ikiwemo kusajili ramani ya eneo hilo na wiki ijayo ofisi ya ardhi itakwenda kukabidhi ardhi kwa vijiji hivyo vitatu pamoja na mwekezaji .

Waziri Lukuvi amesema, kwa sasa ardhi ya shamba hilo imehama kutoka mikono ya kijiji na sasa wananchi wake watapatiwa hati za mjini za miaka 99 yaani hazitatolewa hati za kimila kama ilivyokuwa huko nyuma.

Amesema, Wizara yake italipanga upya eneo la shamba hilo na kusisitiza kuwa wananchi watakaomilikishwa watapaswa kuchangia gharama zote za kupanga, kupima sambamba na zile za miundombinu.

” Halmashauri na serikali ya kijiji mtakaa pamoja na kukokotoa gharama za kuchangia maana tumefanya kazi kubwa ya kuwatafutia ardhi na gharama zenyewe hazitazidi zile za mjini ambazo ni 150,000, pamoja na eneo hilo kupangwa lakini eneo ambalo wananchi wamejenga muda mrefu litarasimishwa” amesema Lukuvi.

Akigeukia suala la ukaguzi mashamba Lukuvi ameagiza kufanyika ukaguzi wa mashamba yote makubwa kwa lengo la kutaka kujua uwekezaji uliyofanyika ikiwemo kujua kiasi yanavyochangia kodi ya serikali pamoja na ajira.

Waziri Lukuvi aliagiza Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Ardhi katila mikoa kufanya ukaguzi wa haraka na kuona kama uwekezaji katika mashamba hayo una tija.

Kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo Mzee Kabongo mkazi wa Ndungu alimshukuru Waziri wa Ardhi kwa kuwezesha kupatikana kwa ekari hizo na kumupmba Lukuvi kufikiria ueezekano wa kuongeza ekari kwa vijiji hivyo.