December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LSF yawapatia msaada wa kisheria watu 175

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WATU takribani 175 wamepatiwa huduma ya msaada wa kisheria waliofika Shirika la Legal Services Facility (LSF) wakati wa Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam.

Wiki ya sheria imehitimishwa leo Jijini Dar es Salaam baada kuzinduliwa Januari 22, 2023, ambapo wadau mbalimbali wa mahakama na sekta ya kisheria walipata nafasi ya kuonesha kazi zao kwa kutoa huduma kupitia maonyesho hayo.

LSF kupitia wasaidizi wa kisheria Jijini Dar es Salaam iliweza kushughulikia mashauri mbalimbali ikiwemo migogoro ya ndoa, matunzo ya watoto, mirathi pamoja na migogoro ya ardhi.

Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa LSF imekuwa ikishirikiana na mahakama kama chombo cha kutoa haki kwa ajili ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania kwa kuwasaidia wananchi kupata haki zao kwa ajili ya maendeleo.

“Wiki ya sheria imekuwa muhimu kwetu kama wadau wa mahakama kwani kupitia wasaidizi wa kisheria tumeweza kutoa huduma bure kwa wananchi waliotembelea banda letu kwa njia ya usulushishi. Kupiti wiki hii tumesaidia watu 175 ambapo wanaume ni 73 na wanawake 102,” ameeleza Ng’wanakilala.

Naye Msuluhishi kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Usuluhishi, Jaji Dkt. Zainab Mango amesema mahakama sasa zinakabiliwa na mashauri mengi yanayoendelea, ambayo pia yanahitaji Ushahidi ili kufanya uamuzi wa mwisho, jambo ambalo hulazimika kuchukua muda mrefu tofauti na kutumia njia ya usulushishi.

“Usuluhishi hauchukui muda mrefu, unachukua muda wa siku 30 tu. Hii ni kwa mujibu wa katiba yetu Ibala ya 107A(1)(d), ambayo inasisitiza kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika mgogoro,” alisema Dkt. Mango.

Dkt. Mango ameendelea kueleza kuwa usuluhishi unapunguza muda mwingi mahakamani na kumpa muda mteja muda wa kufanya shughuli za kiuchumi, kwakuwa katika usuluhishi hakuna dhana ya kila mtu kutaka kushinda, kitu ambacho huleta changamoto kubwa kwenye mashauri yanayoendeshwa mahakamani.

Akiongea kwa niaba ya wasaidizi wa kisheria wengine wanaofadhiliwa na LSF, Anthony Isakwi amesema kuwa wasaidizi wa kisheria wamekuwa wakifanya kazi ya kutatua changamoto mbalimbali katika jamii kwa kutoa hudma za msaada wa kisheria na elimu ya kisheria, ambapo usulushishi umekuwa ukitawala zaidi ili kupata ufumbuzi katika migogoro.

“Usuluhishi imekuwa mbinu yetu kubwa tunayoitumia katika kutatua kesi mbalimbali zinazoripotiwa kwetu. Usuluhishi umekuwa unafanyika zaidi kwenye kesi za madai. Lakini kesi za jinai kama vile ukatili wa kijinsia na kadhalika tunashirikiana na wadau wengine kama vile Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), ambao hupeleka shauri mbele zaidi kwenye vyombo vya utoaji haki ikiwemo mahakama,” amehitimisha msaidizi wa kisheria, Isakwi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho Wiki ya sheria kanda ya Dar es Salaam, yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jijini Dar es Salaam.