January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LSF yapanga mikakati Kampeni ya Mama Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Legal Services Facility (LSF) limeendesha kikao cha kupanga utekelezaji wa kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyozinduliwa Februali 15 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro

Kufuatia uzinduzi huo, LSF limeendesha kikao cha kupanga utekelezaji wa kampeni hiyo katika ofisi zake zilizopo Masaki Jijini Dar es Saalam.

Kikao hicho mahususi kimeratibiwa na Wizara ya Katika na Sheria kwa kushirikisha kikosi kazi kilichojumuisha wadau kutoka serikalini na mashirika yasiyo ya kiserikali kikiwa na lengo kuu la kuangalia utekelezaji wa maeneo makuu matatu ya kampeni hiyo.

Malengo ya Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inalenga kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya utawala wa sheria pamoja na haki za binadamu, kujengea uwezo wadau katika mnyororo wa kutoa haki pamoja na kuboresha mifumo, sera na sheria ili kukuza upatikanaji wa haki nchini.

Akizungumza kuhusu Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni hiyo, Lulu Ng’wanakilala amesema umuhimu wa kampeni hii na jukumu la LSF kama wadau wakubwa katika sekta ya msaada wa kisheria nchini utachochea upatikanaji haki na kuleta nguvu ya pamoja kwa wadau wanaushughulikia masuala ya haki ,usawa na sheria hapa nchini.

“LSF kwa takribani miaka 11 sasa tumekuwa tukitekeleza mradi wa upatikanaji wa haki kwa kuwezesha watoa huduma za msaada wa kisheria zaidi ya 4000 na mashirika 184 Tanzania bara na Zanzibar kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wenye uhitaji bure bila gharama zozote. Kuwepo kwa idadi kubwa ya wasaidizi wa kisheria na mashirika tunayoyapatia ruzuku kumewezesha huduma za msaada wa kisheria kutolewa kila mkoa na kila wilaya;

“Hii imesaidia kupungua kwa migogoro inayoenda mahakamani kwani asilimia 60 ya mashauri takribani 90,000 yanayoletwa kwa watoa huduma za kisheria kila mwaka hutatuliwa na watoa huduma wa msaada wa kisheria. Hii inaonyesha wazi kuwa, mifumo hii ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria na usuluhishi ikiboreshwa zaidi kupitia kampeni hii kwa kiasi kikubwa italeta tija na kuwawezesha wananchi kupata haki zao kwa wakati,” alisema Ng’wanakilala

Aidha Ng’wanakilala aliongeza kuwa, “tunajengea uwezo watoa huduma za msaada wa kisheria kwa kuwapatia kozi mbalimbali za kisheria na haki.

Pia, tunajenga mifumo ya utawala bora, uendeshaji wa kiprogramu na usimamizi wa kifedha kwa mashirika yanayopokea ruzuku kutoka kwetu;

“Hii imesaidia sana kujenga dhana ya uwajibikaji na uwazi kwa mamlaka zinazosimamia shughuli zao na kwa wananchi, ambao ni wanufaika kwa ujumla na kuyawezesha mashirika haya kujidhatiti na kupata rasilimali katika maeneo mengine zitakazowawezesha kufanya huduma za msaada wa kisheria kuwa endelevu,” ameongeza Ng’wanakilala.

Akifafanua zaidi kuhusu jitihada zinazofanywa na LSF ili kutengeneza mfumo endelevu wa kitaasisi katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini amesema kuwa, “Kwa miaka mingi LSF tumekuwa tukiangalia ni kwa namna gani hizi huduma zinaweza kuwa endelevu na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa muda mrefu. Hii ndio sababu ya ushiriki wetu kikamilifu katika ngazi zote za kampeni hii.

“Tuko katika kampeni hii ikiwa ni sehemu ya kufikia matarajio yetu ya kuona kwamba wananchi wanajua haki zao, kunakuwa na mifumo thabiti na uboreshaji wa ushirikiano wa wadau kwa kuchochea juhudi za makusudi kuchukuliwa ili kuboresha sekta ya msaada wa kisheria nchini ikiwemo serikali kutenga rasilimali fedha kupitia mfuko wa huduma za msaada wa kisheria, ambao utafanya huduma hizi kuwa endelevu,” amefafanua Ng’wanakilala.

Makamu Mwenyekiti wa kampeni hiyo, Ng’wanakilala ameomba wadau wote katika sekta ya msaada wa kisheria ikiwemo Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi, pamoja na vyombo vya habari kuunganisha juhudi zao kwa pamoja katika kampeni ili kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya msaada wa kisheria na maisha ya jamii kwa ujumla hususani wanawake na watoto.

“Tunaahidi kuendelea kushirikiana na serikali na wadau katika kuhakikisha tunawafikia watu wengi zaidi hususani maeneo ya pembezoni.” amesisitiza Ng’wanakilala.

Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ilizinduliwa mnamo tarehe 15 Februari 2023, ambapo itaendeshwa kwa takribani miaka mitatu nchi nzima Tanzania bara na Zanzibar.

Makamu Mwenyekiti wa Kampeni ya Huduma ya Msaada ya Kisheria ya Mama Samia, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala (wa kwanza kushoto), akishuhudia uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanywa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro mnamo tarehe 15 Februari 2023 Jijini Dar es Salaam.

Wajumbe wa Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia wakiwa katika kikao kazi maalum kilichoketi kwenye Ofisi za LSF Dar es Salaam chini ya uratibu wa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na wadau wengine ili kupitia mkakati wa utekelezaji kampeni hiyo baada ya kuzinduliwa.