Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
Kamati ya Maadili ya Kitaifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemsimamisha kwa siku saba Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tundu Lissu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa madai ya kukiuka maadili ya uchaguzi.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Kamati ya Maadili ya Kitaifa, Emmanuel Kawishe kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma akieleza kuwa “Leo Oktoba 2, 2020, “kamati imsesikiliza malalamiko dhidi ya Mgombea wa Kiti cha Rais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
“Malalamiko yaliwasilishwa na Chama cha NRA na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Chama cha NRA wakilalamikia kitendo cha mgombea wa kiti cha kiti cha Rais kupitia CHADEMA kutoa maneno ya uchochezi yasiyothibitika. “Ambapo akiwa mkoani Mara, alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ameitisha kikao cha wasimamizi wa uchaguzi nchi nzima ili kuhujumu uchaguzi. Pia imeelezwa kuwa alitoa maneno ya kichochezi na ya kudhalilisha kinyume na maadili ya uchaguzi mkoani Geita,”ameeleza Kawishe.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, barua ya kumtaka Tundu Lissu kujibu tuhuma iliwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA kwa mujibu wa taratibu. “Katibu Mkuu wa CHADEMA alijibu kuwa, malalamiko hayakihusu chama, hivyo, mgombea na chama ni vitu viwili tofauti. Pamoja na kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA alijibu barua ya malalamiko kuwa apelekewe Tundu Lissu mwenyewe, Kamati ya Maadili imeridhika kuwa taarifa kuhusu malalamiko ya ukiukaji wa maadili iliwasilishwa kwa mlalamikiwa kwa mujibu wa taratibu kwa kuzingatia mashariti ya Ibara ya 39 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambapo Bwana Tundu Lissu alidhaminiwa na CHADEMA kugombea kiti cha Rais.Hivyo, barua ya malalamiko kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu ni sahihi kabisa,”amefafanua.
Ameeleza kuwa, Kamati imejiridhisha kuwa, kitendo cha mlalamikiwa kutojibu malalamiko na kuitaka kamati impelekee mgombea malalamiko yeye mwenyewe si sahihi, kwa kuwa malalamiko yote ya maadili yaliwasilishwa kwa Katibu Mkuu na haijawahi kuamuliawa vinginevyo. “Hivyo, wajumbe 11 kati ya 15 wamekubali kuwa malalamiko yamezingatia utaratibu na wajumbe wawili kati ya 15 wamesema uwasilishaji wa malalamiko haukufuata taratibu. Kwa maania hiyo, kamati imeridhia kuwa malalamiko yaliwasilishwa kwa mujibu wa taratibu.
“Baada ya majadiliano ya kina, Kamati imekubali kuwa, Tundu Lissu amekiuka maadili ya uchaguzi kwa kutoa lugha ya kichochezi na tuhuma zisizothibitika kinyume cha kanuni 2.1(a), (b), (d) na (n) na kanuni za maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2020.
“Hivyo, baada ya majadiliano ya kina na uchambuzi wa maadili ya uchaguzi, ambayo wawakilishi wa CHADEMA wameshiriki kikamilifu, Kamati ya Maadili ya Kitaifa imeamua kwa mamlaka iliyopewa chini ya Kanuni ya 5.11(c) na (e) ya Maadili ya Uchaguzi wa Rais , Wabunge na Mdiwani ya mwaka 2020 imemsimamisha kufanya kampeni Tundu Lissu, mgombea kiti cha Rais kupitia CHADEMA kwa siku saba kuanzia tarehe 3 Oktoba, 2020 hadi tarehe 9 Oktoba,2020. Hivyo, mgombea huyo haruhusiwi kufanya kampeni za uchaguzi mpaka atakapomaliza adhabu yake. Ana haki ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa,”imefafanua taarifa hiyo.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi