Na Mwandishi wetu,timesmajira, Online
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimepongeza maamuzi yaliyofanywa na Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuridhia kufufua mchakato wa Katiba Mpya na kueleza maamuzi hayo ni ishara nzuri ya kuimarisha demokrasia na haki za binadamu nchini.
Pia LHRC imetoa mapendekezo ya namna bora ya kuendelea na mchakato wa katiba mpya ili kufanikisha mchakato huo na kuleta matokeo mazuri yanayotarajiwa na Wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Wakili Anna Henga amesema kufanyika mabadiliko ya Sheria yote ya mabadiliko ya Katiba Na. 8/211 na kuweka muundo mpya wa Bunge Maalum la Katiba ili kuanza majadiliano na kutunga Katiba Mpya.
Amesema Bunge linapaswa kutumia Rasimu ya Pili (II) ya Katiba na kueleza ni kutokana kulikuwa na mjadala mkali kuhusu upatikanaji wa Katiba Pendekezwa mwaka 2014.
“Endapo Bunge Maalum la Katiba litaundwa kwa kuweka uwakilishi mpana wa wananchi zaidi ya wabunge kutarudisha imani ya wananchi juu ya mchakato wa katiba na kuwapa uhakika kuwa, masuala ya wananchi yanazingatiwa vyema tofauti na kutanguliza zaidi maslahi ya baadhi ya wanasiasa”amesema Wakili Henga
Amesema njia hiyo itajenga maridhiano na kupunguza tofauti zilizopo kati ya wananchi na viongozi wa siasa.
“Muhimu kukumbuka kuwa mchakato wowote wa kufanya mabadiliko ya katiba ni lazima kuwepo kwa uhuru wa wananchi kushiriki, kuafikiana na kumiliki mchakato wa kuandika katiba, kwani Katiba inapaswa kutokana na ushiriki mkubwa wa wananchi,” amesema Wakili Henga
Aidha ametoa wito kwa Serikali Kupeleka muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kuunda upya Bunge Maalum likiwa na uwakilishi tofauti na wajumbe tofauti na wabunge wachache wa vyama vyote wanaoweza kuwakilishwa.
Amesema Serikali ipeleke mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Kura ya Maoni ili kuipa uhalali wa kisheria sheria hii.
Pia amesema Bunge Maalum la Katiba litakaloundwa litumie Rasimu ya Pili (II) ya Katiba katika majadiliano yake.
Vilevile amesema Serikali inapaswa kuendelea kufungua milango ya majadiliano miongoni mwa watanzania.
Ametaja njia hizo ni pamoja na mikutano, makongamano, midahalo na vyombo vya habari juu ya mambo ya msingi na muhimu ndani ya katiba kwa mstakabari wa taifa letu.
More Stories
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji
Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba