March 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kwaya ya FFC yatoa msaada wa mahitaji mahabusu ya watoto Upanga

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

KWAYA ya Flying Family wameitembelea Mahabusu ya Watoto Upanga na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwa ni sehemu ya upendo na utamaduni wao wa kufanya matendo ya upendo kwa makundi yenye uhitaji.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Meneja wa mahabusu hiyo, Darius Kalijongo, amewashukuru wanakwaya wa kwaya hiyo kwa moyo wao wa upendo na kueleza kuwa msaada huo utasaidia kuboresha mazingira ya malezi kwa watoto walioko mahabusu hapo.

Amesema watoto hao ni wa kila mtu hivyo wanapokumbukwa inasaidia kujisikia vizuri na kuboresha maisha yao wakati wakiwa hapo.

Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Kwaya Ainamringi Foya amesema kuwa wao kama wanakwaya wameguswa na hali ya watoto hao na wameona ni vyema kushiriki katika kuboresha maisha yao.

Amesema wameona ni muhimu kuwafikia watoto hao na kuwapatia msaada huo ambao wanaamini kuwa utawafanya wajisikie kupendwa na kuthaminiwa

Ameongeza kuwa msaada huo unajumuisha baadhi ya vitu ambavyo ni vyerehani viwili, feni, nguo, biskuti, taulo za kike, unga, sukari, mchele, juisi na mafuta ya kupikia ambavyo vitawasaidia watoto hao kuvitumia na kuishi kwa amani.

Aidha kwa upande wa wanakwaya walipongeza hali ya malezi waliyoikuta kwenye kituo hicho kwani picha waliokuwa nayo kabla ya kufika ilikuwa tofauti na hali waliyoikuta.

“Tumefika hapa tumeona watoto hawa wanafundishwa maadili na nidhamu ya hali ya juu na wanaonekana wapo tayari kubadilika, tunaipomngeza taasisi kwa kusimamia na kulinda haki za watoto hawa kwani pamoja na makosa waliyonayo bado wanaendelea kuangaliwa kwa kuzingatia utoto wao,” amesema Innocent Fundisha mwanakwaya na Mwalimu katika kwaya hiyo

Mahabusu ya Watoto Upanga ni kituo maalum kinachotoa huduma kwa watoto wenye tuhuma mbalimbali za jinai, wakiwemo wale ambao kesi zao bado zinaendelea na wale walioko kwenye kipindi cha uangalizi kabla ya kuruhusiwa kurejea kwa jamii.

Kwa sasa kituo hicho kinahudumia watoto tisa wenye umri kati ya miaka 12 hadi 17, ambapo mmoja ni wa kike na wengine nane ni wa kiume.

Kwaya ya FFC inayojumuisha waimbaji kutoka madhehebu mbalimbali ya kikristo wenye vipaji vya uimbaji na imekuwa ni utaratibu wao wa kila mwaka wa kumshukuru Mungu kwa kufanya matendo ya upendo kwa makundi yenye uhitaji mbalimbali.