November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kwagilwa:Shida ya maji Handeni kuwa historia

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Handeni

MBUNGE wa Jimbo la Handeni Mjini mkoani Tanga Reuben Kwagilwa amesema shida ya maji kwenye Mji wa Handeni itakuwa historia baada ya Mradi wa Maji wa Miji 28 kukamilika, kwani mradi huo mkubwa kwa Mkoa wa Tanga utahudumia miji minne ikiwemo Handeni.

Ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara Kata ya Mabanda na kuongeza kuwa mradi huo ni mkubwa na unakwenda kumaliza shida ya maji iliyodumu tangu nchi kupata Uhuru,Miji mingine itakayonufaika na maji hayo ambayo chanzo chake ni Mto Pangani, ni Korogwe, Muheza na Pangani.

“Nataka kuwahakikishia Mradi wetu wa maji wa sh.bilioni 181 unaendelea kujengwa usiku na mchana,pale kwenye chanzo Mswaha (Mto Pangani) wakandarasi wanafanya kazi usiku na mchana ambapo tukishayatoa maji kwenye chanzo yanakwenda kwenye chujio pale Tabora (Korogwe) ambako pia Mkandarasi anafanya kazi usiku na mchana, na tukiyatoa maji kwenye chujio, tutayapeleka Kwamatuku, ambapo napo Wakandarasi wapo site.

“Baada ya hapo yatasukumwa Sindeni na baada ya hapo maji yatasukumwa kwenda Mlima Mhandeni,kwa sasa tenki la Mlima Mhandeni limefikia kwenye hatua ya kulifunika,nalo bwawa la Kwemkambala ujenzi wake unaendelea usiku na mchana, na kabla ya mvua za vuli, bwawa la Kwemkambala litakuwa limekamilika na mvua za masika zikinyesha zitajaza bwawa la Kwemkambala, tutayachukua maji kutoka bwawa la Kwemkambala hadi Mlima Mhandeni, hivyo mwakani mwanzoni Handeni itakuwa na maji” amesema Kwagilwa.

Kwagilwa amesema kazi hiyo iliyotukuka ni ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuwaondolea adha ya maji wananchi wa Handeni na kwa Rais Dkt. Samia kuwapelekea maji wananchi wa Handeni, ataingia kwenye Kitabu cha Kumbukumbu za Guinness (Guinness World Record).

“Baada ya hapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ataingia kwenye Kitabu cha Maajabu ya Dunia cha Guinness kwa kuyaleta maji Handeni mahali ambapo wananchi wake wamekuwa na dhiki ya maji kwa miaka mingi sana.

“Tunakwenda kuiandika historia kwa pamoja wewe (mwananchi) na mimi na siku si nyingi mtaona wataalamu wanapita kwenye mitaa yenu kwa ajili ya kuunganisha mabomba kwa kuwekwa ndani mwenu au kwenye vituo vya kuchota maji vya umma (vilula)” amesema Kwagilwa.

Kwagilwa amesema jambo jingine kubwa kwenye Kata ya Mabanda ni ujenzi wa kituo cha afya hivyo kituo hicho kitajengwa ili kuwaondolea adha wananchi ya kufuata huduma za matibabu mbali, huku akitanabaisha kuwa umeme umeshafika maeneo ambayo hayakutarajiwa kufika.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge amesema Rais Dkt.Samia amedhamiria kuboresha huduma za jamii na shughuli za maendeleo kwa kupeleka fedha nyingi za miradi vijijini ikiwemo miundombinu ya maji, barabara, shule na vituo vya afya.

Mhandisi Ulenge amesema, bado anahakikisha anatoa fursa za kiuchumi kwa kuweka mazingira mazuri kwa wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali, hivyo wananchi wanatakiwa kumuunga mkono na kumtia moyo kwa mambo yote anayofanya kwenye nchi hii kwa ajili ya wananchi wake.