Na Penina Malundo na Bakari Lulela
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea amesema hana mpango wa kuhama CHADEMA kwa kisingizio cha kumfuata rafiki wake wa karibu Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Anthony Komu .
Amesisitiza kwamba yeye bado ni mwanachama halali wa chama hicho na anaongoza jimbo lake kwa mujibu wa Sheria na Katibu kwa kufanya kazi za wananchi wake waliomchagua. Kubenea alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kile alichokiita uzushi kuwa anataka kuhama chama CHADEMA.
Alisema yenye ni kada wa CHADEMA na kazi aliyonayo ni kuiheshimu na kuilinda katiba ya chama chake. Alifafanua kwamba anashangazwa na uvumi huo kuwa yeye anataka kuondoka katika chama hicho, jambo lisilo na ukweli kwani yeye bado ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo na jukumu lake ni kuhakikisha anawasimamia wananchi wake wa jimbo la ubungo.
“Tuhuma zinazohusiana na kuhama kwangu CHADEMA kumfuata rafiki yangu wa siku nyingi Komu baada kuondoka kwake CHADEMA kusema ukweli si kweli,” alisema na kuongeza;
“Ni kweli (Komu) ni rafiki yangu tumefanya mambo mengi pamoja iwe ya kisiasa ama ya kijamii hivyo kuondoka kwake katika chama cha CHADEMA isiwe suluhisho la watu kuongea mambo mengi yasiyo kuwa na kichwa wala miguu.”
Alisema kumekuwa na maneno yasiyo na ukweli kutoka kwa watu aliowaita wapiga ramli kueneza habari ambazo si za kweli na zikimuhusisha yeye na kuwataka waache uzushi huo.
“Kumekuwa na taarifa za uzushi zilizotengenezwa na kuenezwa katika mitandao ya kijamii na watu ambao si wema wakielezea tukio la kuondoka kwangu CHADEMA. Habari hizo hazina ukweli wowote mimi bado mwanachama halali wa chama hicho,” alisema Kubenea
Katika hatua nyingine mbunge huyo ameiomba Serikali kuhakikisha inaungana na viongozi mbalimbali wakiwemo wa upinzani kuendeleza jitihada za uwekaji tahadhari zitokanazo na maambukizi ya virusi vya Corona kwa Watanzania.
Alisema wananchi wa Jimbo la Ubungo wanahatari zaidi ya kupata ugonjwa wa Corona kutokana na mikusanyiko ya watu katika maeneo ya mabasi ya mwendokasi na baadhi ya vituo vya magari yanayopokea abiria wengi kutoka nje ya nchi kuwepo kwenye eneo hilo.
“Nilikuwa Bungeni, lakini nimelazimika kurudi baada ya kuona msongamano wa watu wakiwa katika vituo vya mwendokasi wakisubili huduma ya usafiri hiyo ni hatari kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona kuikumba nchi yetu,” alisema Mbunge huyo
Mbunge huyo ameitaka jamii kuwa makini na janga hilo kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na sehemu zenye kuhitaji watu wengi ikiwemo kwenye mazishi na nyumba za ibada watu wakajipanga kwa uchache ili kukamilisha suala husika.
Kutokana tahadhari hiyo ya Corona aliwataka viongozi wa dini zote kuweka taratibu nzuri za ibada ikiwezekana kwa kupeana zamu kwa kuepuka msongamano isiyokuwa na lazima ili kuepuka maambukizi ya ugonjwa huo.
Kubenea alimshukuru Spika wa Bungem Job Ndugai kwa kuweka utaratibu mzuri wa uendeshaji wa vikao vya Bunge wenye kuchukua tahathari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
More Stories
Balozi Kombo :Maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu nishati yakamilika, Marais 25 kuhudhuria
Mbunge Mavunde awawezesha kiuchumi wafanyabiashara soko la Sabasaba Dodoma
Msama: Geor Davie ni mtumishi wa kweli