Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online
NAIBU Waziri wa kilimo Anthony Mavunde ameshuhudia mzigo wa korosho zaidi ya tani 7 zikisafirishwa na kampuni ya Ward Holding Tanzania (WHT) kwenda kuuzwa nchini marekani, lengo ni kuhakikisha asilimia 60 ya korosho zote zinazozalishwa na zinabanguliwa ifikapo msimu wa mwaka 2025/2026.
Akizungumza wakati wa kushuhudia mzigo huo Naibu Waziri wa kilimo Anthony Mavunde Oktoba 31, 2022 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amesema kuwa Leo tunashuhudia tukio la kihistoria, ambapo korosho iliyobanguliwa nchini Tanzania inaenda kuuzwa kwa mtumiaji wa mwisho nchini Marekani.
“hii ni habari njema kwa wakulima wa korosho nchini ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan ya kufungua nchi kimataifa, hali inayopelekea kuongeza uhakika wa masoko ya mazao ya wakulima wetu” amesema Mavunde.
“Kila kitu katika bidhaa hii, kuanzia kuibangua na kuiweka kwenye vifungashio vinavyovutia imefanywa hapa hapa Tanzania, hakika Watanzania tunaweza, Nitoe rai kwa Taasisi za fedha kuendelea kuunga mkono juhudi za wajasiriamali na sekta binafsi kwa ujumla ili iendelee kukua na kuwa na mchango chanya kama huu kwenye maendeleo ya sekta ya kilimo na nchi kwa ujumla” amesema Mavunde
Bei ya korosho ghafi nchini ni kati ya 1,800 hadi 2,200 ambapo unahitaji kilo tano za korosho ghafi ili kupata kilo moja ya korosho iliyobanguliwa. Wakati huo huo, bei ya korosho iliyobanguliwa nchini Marekani ni Dola za Kimarekani 40 (sawa na zaidi ya shilingi 90,000 za Kitanzania), hesabu hii inaonesha dhahiri kuwa kuuza korosho iliyobanguliwa kuna manufaa makubwa kwa wakulima wetu na Taifa kwa ujumla.
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Chama cha Wabanguaji Korosho Tanzania ili kuhakikisha tunakuza tasnia ya Korosho kwa kuongeza thamani hali itakayosaidia kuongeza kipato kwa wakulima na kuongeza mchango wa zao la korosho katika kukuza uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake Rais wa Kampuni ya Ward Holding Tanzania, Godfrey Simbeye ameeleza kuwa mahitaji ya korosho iliyobanguliwa nchini Marekani ni karibu mara 4 ya korosho tunayozalisha nchini kwa sasa, hivyo fursa ya soko ni kubwa, lenye faida zaidi kwa mkulima na Taifa kwa ujumla ukilinganisha na uuzaji wa korosho ghafi.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Robert Raines ameihakikishia nchi ya Tanzania katika ushirikiano wa kutosha ili kuwawezesha wakulima wa korosho kupata soko la uhakika nchini Marekani.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu