January 25, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Korea yaonesha utayari kuwekeza nchini katika uendelezaji wa madini mkakati

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Serikali imesema tayari kushirikiana na Jamhuri ya Korea katika kutekeleza mkakati wake wa kuendeleza madini mkakati na muhimu nchini.

Hayo yamesemwa leo tarehe 24 Januari, 2025 na Waziri wa Madini, Mh.Anthony Mavunde alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mh.Eunju Ahn katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

“Mh.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupa maelekezo mahsusi ya kuhakikisha rasilimali hii ya madini mkakati tunaiwekea mfumo thabiti ili Nchi yetu ipate manufaa zaidi,Mkakati wa uvunaji madini ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika umelenga kutimiza adhma hiyo ya Rais wetu.

“Mojawapo ya nguzo mbili muhimu katika Mkakati huo ni kufanya utafiti wa kina ili kutambua aina na kiasi cha madini mkakati kilichopo, pamoja na kuweka mazingira rafiki ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini hayo hapa nchini.

Tanzania ni moja ya Nchi chache duniani ambazo zimebarikiwa na uwepo wa madini ya aina zote na kutoa wito kwa wawekezaji kutoka nchini Korea kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini nchini“Amesema Mavunde

Awali, akieleza lengo la kuomba miadi hiyo, Balozi Ahn ameeleza lengo hasa ni kujitambulisha kutokana na mahusiano ya siku nyingi ya Korea na Tanzania, hususani katika sekta ya madini, na kusisitiza kwamba yupo tayari kuhakikisha mashirikiano hayo yanakuwa na tija kwa nchi zote mbili katika kuendeleza sekta ya madini hususan madini mkakati na kwakuwa tayari kampuni ya POSCO kutoka Korea imeonesha utayari wa kushiriki kwenye mradi wa madini kinywe wa Mahenge,Mkoani Morogoro.