January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar

Na Jackline Martin,TimesMajira Online

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ubelgiji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ZIPA, na TPSF, wameendesha Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji.

Akizungumza wakati akifungua kongamano hilo leo Jijini Dar es Salaam Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amesema kuwa ushirikiano huo utachochea dhima ya serikali ya Tanzania ya kufikia kille cha uchumi wa viwanda.

Amesema hadi sasa Tanzania imesafirisha bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Dola milioni 186 nchini Ubelgiji huku nchi hiyo ikiingiza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 115 ambapo mkakati wa serikali ni kuongeza uwekezaji zaidi.

Ameendelea kusema kuwa Tanzanua husafirisha zaidi bidhaa za kilimo kwenda nchini Ubelgiji ikiwemo Chai, Kahawa huku sekta nyingine ikiwa ni madini.

Mbali na hayo Dkt. Jafo amesema watanyabiashara kutoka Ubelgiji watatembelea maeneo
mbalimbali ya uwekezaji chini Tanzania, ikiwa ni pamoja na Bandari na visiwa vya Zanzibar, ili kuona fursa za uwekezaji zinazopatikana.

Dkt. Jafo ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji
Watanzania kutumia fursa hii ya kukutana na wenzao kutoka Ubelgiji ili kukuza biashara zao na kupata masoko kwa mazao yao na bidhaa mbalimbali nje ya mipaka ya Tanzania.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Abouk Nyamanga, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ubelgiji umeleta matokeo chanya, hasa katika sekta ya madini, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya madini ya almasi kutoka Tanzania yanauzwa nchini Ubelgiji kupitia bandari za Tanzania.

Naye, Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Mhe. Peter Hyughebaert, ameeleza kuwa mkutano huu ni matokeo ya kikao kilichofanyika mwaka 2022 kati ya Umoja wa Mataifa ya Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa ya Ulaya (EU) mjini Brussels, Ubelgiji, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Mhe. Alexander De Croo, kujadili namna ya kuimarisha biashara na mahusiano kati ya Tanzania na Ubelgiji.

Mkutano huo pia ulijumuisha taasisi na makampuni mbalimbali kutoka Tanzania na Ubelgiji, ambayo yalishiriki katika kutambua vivutio vya kibiashara na kiuwekezaji vilivyopo katika nchi hizo
mbili.