Na Joyce Kasiki,Timesmajira ,Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Kodi kwa mwaka 2023 linalotarajiwa kufanyika Januari 11 mwaka huu jijini Dar Es Salaam huku wafanyabiashara zaidi ya 300 wakitarajiwa kushiriki katika kongamano hilo lililolenga kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 04,2023 jijini Dodoma Kamishna wa Sera ,Wizara ya Fedha na Mipango Elija Mwandumbya Mwandumbya amewaasa wadau watakaoshiriki katika kongamano hilo kutoa michango na maoni yao kwa lengo la kuboresha sera za nchi na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi ,biashara na uwekezaji hapa nchini.
Amesema,wadau wanaolengwa kwenye kongamano hilo ni wale wa kutoka sekta binafsi wakijumuisha wakurugenzi ,Mameneja ,Watalaam wa Kodi,wafanyabiashara ,Makundi Maalum pamoja na Mabalozi mbalimbali nchini ambapo amesema kongamano hilo litaongozwa na kaulimbiu isemayo’ ‘Maboresho ya Sera kwa Mandeleo ya Watu’.
Mwandumbya amesema tukio hilo ni la kipekee litkalokutanisha wataalam wa uchumi ,fedha na kodi nchini kutoka Serikalini na sekta binafsi ili kujadili mustakabali wa nchi katika kukuza uchumi,biashara,uwekezaji na hatimaye kuongeza mapato ya serikali.
Ametaja baadhi ya mada zitakazozungumzwa katika kongamano hilo kuwa ni pamoja na hali ya uchumi Duniani,fursa na athari zake kwenye sera za uchumi ,uwekezaji na biashara hapa nchini na Mfumo wa kodi ,ada na tozo hapa nchini na hali ya ulipaji kodi wa hiari.
Mada nyingine ni changamoto za ulipaji kodi wa hiari katika mazingira ya uchumi ,biashara na uwekezaji nchini hapa nchini na mchango wa sekta ya fedha katika kukuza uchumi ,biashara na uwekezaji hasa wakati huu wa changamoto za uchumi Duniani.
Kwa mujibu wa Mwandumbya jukumu la Wizara ya Fedha na Mipango katika kongamano hilo ni kusikiliza na kukusanya maoni kwa nia ya kuboresha uratibu wa maoni na kuongeza ushirikishwaji wa makundi hayo katika utunzi wa sheria.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024