Na Allan Vicent, TimesMajira Online
MWANAFUNZI wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) tawi la Tabora Happy Marko (23) aliyekuwa na tatizo la kutosikia kwa zaidi ya miaka 12 amefunguliwa katika mkutano wa injili na kuanza kusikia tena.
Mwanafunzi huyo anayesoma shahada ya kwanza ya ualimu (elimu maalumu) amepata muujiza huo baada ya kuombewa na Mhubiri wa Kimataifa na Mwinjilisti Askofu Simon Masunga katika mkutano wa injili uliofanyika katika viwanja vya kanisa la TAG Kitete Christian Center mjini Tabora.
Akihojiwa na mwandishi wa gazeti hili, Happy alisema alipata tatizo hilo akiwa na umri wa miaka 11 alipokuwa anasoma kidato cha 1 katika shule ya sekondari Nyabulogoya iliyoko jijini Mwanza.
Alisema tatizo la kutosikia lilianza kidogo kidogo na hakujua nini kimeingia masikioni mwake na baada ya muda akapoteza usikivu katika masikio yake yote mawili hadi alipoombewa na mtumishi wa Bwana Askofu Masunga.
Alibainisha kuwa katika kipindi chote cha masomo yake ya sekondari, kidato cha tano na sita hadi chuo kikuu alikuwa anasoma kwa usaidizi (elimu maalumu) na hata katika masomo yake ya Chuo Kikuu anasoma shahada ya kwanza mchepuo wa elimu maalumu.
‘Namshukuru sana Mungu kwa kunifungua, nitaendelea kumtumikia katika maisha yangu yote, nilikuwa nasali kanisa katoliki lakini kuanza sasa nitaungana na wapendwa wenzangu hapa Kitete Christian Centre (KCC)’, alisema.
Happy aliwataka wanafunzi wote wenye tatizo kama lake na mengineyo kumwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha ili aweze kuwaponya na kuwafungua vifungo vyote vilivyoko katika miili yao.
Mhubiri wa mkutano huo Askofu Rev Masunga kutoka Mkoani Geita alisema neema ipo kwa ajili ya kuokoa na kufungua wote waliofungwa na nguvu za giza hivyo akaitaka jamii kumgeukia Mungu ili isiendelee kuteseka.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua