Na Pius Ntiga, TimesMajira Online, Same
KILIO cha muda mrefu cha wananchi wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro cha kupata Kiwanda cha kchakata Tangawizi sasa kimepata ufumbuzi na kitaanza kufanya kazi Novemba mwaka huu baada ya kupata Mwekezaji.
Kiwanda hicho kilichoanzishwa Mwaka 2012, kilifanya kazi kwa muda mfupi kikaharibika chini ya Chama cha Ushirika cha Tangawizi Mamba, Miamba, ambapo sasa kimeingia ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii-PSSSF na kitaanza kufanya kazi Novemba mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uwekezaji-PSSSF, Fortunatus Magambo katika Kata ya Mamba, Miamba wakati akikabidhi rasmi mashine za muchakata Tangawizi zilizotolewa na Mfuko huo mbele ya mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule
Katika mkutano na wananchi ambao ulihudhuriwa pia na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM Kijijini hapo, Magambo amesema mashine hizo za kisasa zimenunuliwa nchini China kwa gharama ya shilingi Bilioni-1.83 na zinafanya kazi bila kutoa Suti.
Kwa mujibu wa ubia huo PSSSF ina hisa ya asilimia 60 huku 40 zikiwa ni za Wananchi wa Wilaya ya Same ambao zao lao kuu la Biashara ukiachia Mkonge ni Tangawizi.
Amesema, kiasi cha shilingi milioni 800 zitatumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya kiwanda, Ofisi, Hospitali, Karakana na Miundombinu pamoja na matumizi ya awali ya kiwanda hicho.
“Tunataka kuona mradi huu unakamilika na kusaidia kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Same na utakamilika kwa wakati. Wataalamu kutoka China wanatarajiwa kuwasili nchini Oktoba mwaka huu kwa ajili ya kufunga Mashine hizi tayari kwa kuanza uzalishaji.” Amesema Magambo.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule, amewaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa serikali ya awamu tano imejipambanua kuwa ni Tanzania ya Viwanda, hivyo uwepo wa kiwanda hicho utachochea kukuza vipato vyao na Taifa kwa ujumla.
Amesema, tani 5,000 kwa mwaka zinahitajika kiwandani hapo, hivyo akawataka wakulima kuongeza uzalishaji wa Tangawizi ambayo itakuwa inasindikwa hapa hapa nchini kwa matumizi ya hapa nchini na nje ya nchi.
Aidha, DC Rosemary amesema Soko la Tangawizi litakuwa kubwa mara kitakapoanza uzalishaji kiwanda hicho cha kusindika Tangawizi, Same.
Pia amewataka wananchi kuwapuuza Wanasiasa wakiwemo wa upinzani wanaojipitisha kwao wakidai kuwa mashine za kiwanda hicho wamezileta wao wakati zimeletwa na serikali ya awamu ya Tano.
“Wananchi wangu wa Same hasa hapa Mamba, Miamba, Corona ilichelewesha ufungaji wa mashine hizo lakini sasa zipo hapa na nyie leo mmeshuhudia, hivyo muda wowote zitaanza kufanya kazi, endeleeni kuiunga mkono serikali yenu” amesema DC Rosemary
Wakizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM, baadhi ya wananchi akiwemo Mzee Ndimangwa Manento, aliyetoa Shamba lake kwa ajili ya kujengewa kiwanda hicho cha Tangawizi, wameishukuru serikali kwa kusikiliza kilio chao cha kuleta mashine za kisasa zisizo na Sauti na wakawaomba wananchi wenzao mwaka huu wasifanye makosa katika Uchaguzi mkuu wakampigie kula nyingi Dkt. John Magufuli, Wabunge na Madiwani wa CCM.
Wakati huo huo, zaidi ya shilingi milioni 400 zimetumika kujenga majengo mapya ya kituo cha afya cha Ndungu ikiwemo maabara, chumba cha kuhifadhi Maiti, jengo la Upasuaji, pamoja na Wodi ya Akina mama wajawazito.
Kaimu Mganga Mkuu kituo hicho cha Afya cha Ndungu, Hamis Waziri Juma amesema, kabla ya majengo hayo walikuwa wanatoa rufaa nyingi kwenda Hospitali ya Wilaya ya Same kwa ajili ya matibabu, lakini sasa wajawazito wanajifungua katika kituo hicho na hivyo kupunguza gharama ya wanachi kuwapeleka Same.
Katika hatua nyingine, zaidi ya shilingi milioni 60 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa Shule Kongwe ya Same Sekondari katika miaka mitano ya serikali ya Tano chini ya Rais Magufuli.
Mkuu wa Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 Hoza Mgonja amesema, majengo 24 yamekarabatiwa yakiwemo mabweni, jiko, madarasa, maabara, zahanati, ofisi na kujenga T]tenki la maji kwa ajili ya matumizi ya Shule hiyo ambayo sasa ni ya kidato cha Tano na Sita.
Wakizungumzia mafanikio hayo baadhi ya wanafunzi wamesema kuwa, shule hiyo sasa imekuwa ya kisasa baada ya majengo ya zamani kubadilishwa na kujengwa mapya imesaidia pia kuongeza ufaulu na walimu kufundisha katika mazingira mazuri na wameipongeza Serikali.
Aidha, shilingi milioni 25 zimepelekwa na serikali kukarabati na kujenga ofisi na madarasa mawili katika shule ya sekondari Mamba, iliyopo Kata ya Mamba, Miamba Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
Kiasi hicho cha fedha kimetajwa na mkuu wa shule hiyo Elizabet Irira, ambaye pia ameipongeza serikali kwa kupeleka kiasi hicho cha fedha shuleni hapo, hatua ambayo pia imepongezwa na wanafunzi wa shule hiyo iliyopo milimani kilometa 90 kutoka Mjini Same hadi Mamba, Miamba.
More Stories
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo