Na Martha Fatael,TimesMajira online
GAWIO kutoka katika mashirika ya umma ni wimbo uliokosa waimbaji
awali, kwani asilimia kubwa ya mashirika hayo yalikuwa yakiripoti
kupata faida ndogo na mengine hasara na hivyo kushindwa kupeleka gawio
kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo.
Ilikuwa ni kama mazoea kutosikia taarifa za kuwapo kwa Gawio kutoka
katika taasisi mbalimbali za umma na kampuni ambazo serikali ina hisa.
Mara baada ya kuingia kwa serikali ya awamu ya tano, Chini ya
aliyekuwa rais Hayati Dk John Pombe Magufuli,Serikali yake
ilijielekeza katika ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwamo ya
Bwawa la kufua Umeme la Mwalimu Nyerere na ununuzi wa Ndege.
Miradi mingine ni pamoja na Miundombinu ya barabara, Madaraja ya juu
(Flyover), Reli ya Kisasa ya SGR, Vituo vya mabasi, Upanuzi wa viwanja
vya ndege, Ujenzi wa Vituo vya afya, Maji, Elimu na hospitali sanjari
na Usambazaji wa umeme vijijini.
Kwa pamoja,miradi hiyo inahitaji fedha nyingi ambazo serikali chini
ya hayati Dk Magufuli haikuwa na namna nyingine zaidi ya kuzibana
taasisi na kampuni ambazo imewekeza hisa zake kuhakikisha
yanajiendesha kwa faida lakini yanatoa gawio kulingana na mikataba
yao.
Ni katika muktadha huo,mwaka 2019, wakati wa uhai wake, aliyekuwa
Rais wa Awamu ya Tano, Dkt.Magufuli alipokea kiasi cha shilingi
Trilioni 1.05 zinazotokana na gawio na michango kutoka taasisi,
mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa.
Katika taarifa yake Msajili wa Hazina, Athuman Mbuttuka anasema
fedha za gawio na michango iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli ni ya mwaka wa
fedha wa 2018/19 na imetoka katika taasisi, mashirika ya umma na
kampuni 79 kati ya taasisi, mashirika ya umma na kampuni zote 266
ambazo Serikali imewekeza mitaji.
Anasema kiasi hicho kimeongezeka kutoka shilingi Bilioni 161.04
zilizokusanywa katika mwaka 2014/15.
Kutokana na juhudi hizo,idadi ya taasisi, mashirika ya umma na
kampuni zinazotoa gawio na michango zimeongezeka kutoka 24 mwaka
2014/15 hadi kufikia 79 mwaka 2018/19.
Akifanya ziara katika Kiwanda cha Sukari TPC Ltd,Waziri wa Kilimo
Prof Adolf Mkenda anaipongeza menejimenti ya kiwanda hicho kutokana na
taarifa yake ya kutoa gawio la zaidi ya Sh.Bil. 15 kwa mwaka 2020.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kiwandani hapo na kumnukuu, Afisa
mtendaji mkuu, Robert Baisac, Inaeleza TPC ilianzishwa mwanzoni mwa
mwaka 1930, kwa jina la A/S Tanganyika planting Company limited na
A.P Moller mfanyabiashara wa Denmark na ilisajiliwa rasmi nchini kama
TPC Ltd mwaka 1973.
Ilipofika Machi 2000, TPC Ltd ilikuwa imebinafsishwa kwa shirika la
uwekezaji lwa Sukari likijulikana kwa Kiingereza Sukari Investment
Limited (SIL) ambayo ilinunua Hisa asilimia 75 katika kampuni ambapo
asilimia 25 iliyobaki ilishikiliwa na serikali.
Mchango wa TPC kwa uchumi kupitia kodi, kama vile kodi ya huduma
(Service Levy),Kodi ya ongezeko la thamani (VAT),Payee na kodi ya
maendeleo ya shule zilifikia jumla ya Sh.Bil.68.4 mwaka 2017
ikilinganishwa na Sh.Bil.1.6 zilizorekodiwa mwaka 2000.
Anasema mchango wa TPC Ltd kwa Serikali kwa maana ya Gawio ilikuwa
kati ya Sh.Bil.13.429 mwaka 2017 na kwamba gawio kwa Serikali tangu
mwaka 2004 hadi 2019 ni Sh.Bil 74.
Mara baada ya taarifa hiyo, Pro.Mkenda anaipongeza TPC kwa kutoa Gawio
la kiasi cha Sh.Bil.15.5 kiasi ambacho si viwanda vyote vilivyoweza
kutoa kiwanga hicho.
Anasema kiwanda cha Kilombero pamoja na ukubwa wake na Serikali kuwa
na hisa ya asilimia 25 bado hawajatoa gawio kubwa kama la TPC.
Prof.Mkenda anasema Gawio linalotolewa na TPC ni zaidi ya mara mbili
ikilinganshwa na lile linalotolewa na kiwanda cha Kilombero mkoani
Morogoro.
Mapema akitoa taarifa kwa waziri Mkenda,Afisa mtendaji Utawala wa
TPC,Jaffary Ally anasema TPC ni kwanda cha Mfano ambapo wamekuwa na
mafanikio makubwa kwa kuongeza uzalishaji kutoka tani 36,000 mwaka
2000 wakati wanabinafsisha hadi tani 110,000 kinachozalishwa sasa.
Kwa mwaka huu wamezalisha tani 103,000 na kupita malengo ya msimu
uliopita wa kuzalisha Tani 95,000 ambao ulipata changamoto ya mwaka
jana kwani walikumbwa na mafuriko na hivyo kuathiri baadhi ya mashama
ya miwa sanjari na kuwa na ugonjwa wa Yellow sugar cane.
Anasema mafanikio yanayopatikana yanatokana na kiwanda kuwekeza mtaji
wa zaidi ya Sh. Bil.226 ambazo zimetumika katika kuongeza uwezo wa
kiwanda katika kuchakata miwa,uwezo wa mashamba katika kutoa miwa
zaidi ambapo sasa utoaji wa miwa umefikia takribani Tani 140 kwa Hekta
moja.
Ally anasema kiwango hicho ni bora miongoni mwa nchi zote
zinazozalisha miwa duniani huku pia kiwango hicho ni moja kati ya
viwango bora vitatu vya uzalishaji wa miwa duniani.
Anasema waziri ameridhiwa na jinsi kiwanda cha TPC kinavyoweza
kukabiliana na ushindani wa uzalishaji wa sukari duniani.
Hata hivyo, Ally anasema jududi zinazoonekana sasa katika kiwanda cha
TPC zinazotoakana na mazingira wezeshi yaliyoandaliwa na iliyokuwa
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya aliyekuwa Rais,Hayati Dkt.Magufuli.
Anasema serikali ilitumia vyombo vyake mbalimbali katika kuhakikisha
viwanda vya ndani vinalidwa kikiwamo cha TPC huku Hayati Magufuli
akisiitiza suala la taasisi na kampuni hizo kutoa gawio kwa serikali
kama njia kuu ya kuchangia uchumi wa Taifa.
Mnamo mwaka 2019, wakati wa Uhai wake, Hayati Dkt.Magufuli wakati
akipokea gawio la Trilioni 1.05, alizipongeza taasisi, mashirika ya
umma na kampuni 79 zilizotoa gawio na michango kwa Serikali.
Aidha Magufuli alitaka taasisi, mashirika ya umma na kampuni 187
ambazo hazikutoa gawio na michango kwa wakati huo, kutoa gawio na
michango hiyo vinginevyo bodi zake zitavunjwa na uteuzi wa watendaji
wakuu kutenguliwa.
Rais Magufuli alifafanua kuwa Serikali imewekeza mitaji ya kiasi cha
shilingi Trilioni 59.6 katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni
266 ikitarajiwa kuwa zitaendeshwa kwa tija badala ya kuwa tegemezi kwa
Serikali ama kuendeshwa kwa hasara.
Dkt.Magufuli anasema kulikuwa na jumla ya mashirika, taasisi na
makampuni karibu 266 lakini ukiangalia walioleta ni 79, yapo mengine
187 hayajaleta, na kumuagiza aliyekuwa waziri wa fedha kwa mwaka 2019,
ambaye sasa ni makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango awahimize mashirika
hayo kutoa gawio kabla ya hatua kuchukuliwa.
Akizungumza na taasisi hizo, alitaja takwimu kuhusu suala la Gawio
ambapo alisema, ndani ya miaka mitano kuanzia 2014-15 mashirikia,
taasisi na makampuni yaliyotoa gawio yalikuwa ni 24 na walikabidhi
jumla ya shilingi Bilioni 130.
Mwaka 2015-16 yalikuwa 25 na yalikabidhi shilingi bilion 249, mwaka
2016-17 yalipanda hadi kufikia 38 na wakatoa gawio la shilingi bilioni
677 na kwa mwaka 2017-18 yalikuwa 40 na wakakabidhi shilingi bilioni
842.
Pia kwa mwaka 2018-19 mashirika, makampuni na taasisi zimepanda hadi
kufikia 79 wakitoa jumla ya shilingi Trilioni 1.05.
Serikali ilisisitiza kuwa utendaji kazi wa taasisi hizo ni moja kati
ya vyanzo muhimu vinavyopaswa kuchangia katika maendeleo ya nchini
ikiwemo miradi mikubwa inayotekelezwa nchini, na amerejea kauli yake
kuwa kutokana na fursa zilizopo hapa nchini zikiwemo maji, ardhi,
madini, gesi, mifugo na nguvu kazi, hakuna sababu ya Watanzania
kujiona masikini.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu