April 14, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kituo cha Afya Makojo kuondoa changamoto ya umbali wakazi zaidi ya  20,000,Musoma Vijijini

Fresha Kinasa TimesMajira Online Mara.

WAKAZI zaidi ya 20,000 wa Vijiji vya Chimati,Chitare na Makojo Kata ya Makojo  Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara,  wameondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu takribani kilometa 20 kufuata Huduma za Afya katika Kituo cha Afya Murangi.

Ni baada ya kuzinduliwa utoaji wa Huduma za Afya kwenye Kituo Kipya cha Afya cha Kata ya Makojo (Vijiji vya Chimati, Chitare na Makojo).Uzinduzi huo   ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka na kuhudhuriwa na Wananchi wa Vijiji hivyo na Viongozi mbalimbali  wa serikali.

Akizungumza Wakati wa uzinduzi wa Kituo hicho,Machi 7,2025 Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka amesema kuwa kituo hicho kitakuwa  mkombozi kwa Wananchi hao ambapo awali walipata adha ya  kutembea umbali kufuata Huduma za matibabu.

“Kutoka kwenye kilindi cha moyo wangu, namshukuru Sana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambazo zimesaidia ujenzi wa Kituo hiki.Tafsiri yake ni kwamba, Mama anawapenda Wananchi kwa dhati kabisa.Tuendelee kumuunga mkono Rais wetu kwa kazi kubwa na nzuri anazozifanya,”amesema Chikoka.

“Namshukuru Rais Dkt.Samia kwa kutoa Mil. 500,kutujengea kituo hiki cha Afya ambacho kitatuhudumia karibu na makazi yetu.Tulikuwa tunatembea umbali mrefu kwenda Kituo cha Afya Murangi lakini kwa sasa tutatibiwa bila usumbufu kama ilivyokuwa awali,”amesema Rhoda Paulo Mkazi wa Kijiji cha Chimati. 

Mujungu Misana ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Makojo ameishukuru serikali kujenga kituo hicho kwani kitaokoa pia muda ambao wananchi waliutumia kutembea umbali mrefu kufuata matibabu,muda huo utatumika kwa shughuli za uzalishaji mali.

Neema Bwire Mkazi wa Chitare amesema kituo hicho kitakuwa mkombozi kwa kina hasa kina Mama Wajawazito wakati wa kujifungua na kupata Huduma bora hali ambayo itawafanya wawe salama kwa kujifungulia kituoni hapo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma,Musongela Palela amesema kuwa Kituo hicho ni cha Kimkakati kitasaidia kupunguza vifo vya Mama na mtoto na pia kuondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu wa takribani kilometa 20 kwenda kupata huduma kituo cha Afya Murangi.” amesema Musongela.

Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21 zenye jumla ya vijiji 68 kwa sasa,lina
Hospitali ya Halmashauri yenye vifaa vya kisasa vya matibabu ikiwemo complete radiology unit (mobile digital X-ray & static X-ray), oxygen-production plant, na Mashine mbili za Ultrasound.
Huku pia  likiwa na  Vituo sita vya Afya vikiwa na vifaatiba vya kisasa.

Aidha,Vituo hivyo ni Bugwema, Kiriba, Kisiwa cha Rukuba, Makojo, Mugango na Murangi.

Ambapo zipo  Zahanati 26 za Serikali na nne za binafsi,Zahanati 17 mpya zinajengwa vijiji mbalimbali jimboni humo kwa nguvu za wananchi na nyingine zimeanza kupokea misaada ya kifedha kutoka Serikalini.

Pia,Magari ya Wagonjwa (Ambulance) ni saba likiwemo gari kubwa la kisasa kutoka Japan lenye vifaa vya upasuaji ambalo liko kwenye Kituo cha Afya cha Murangi.

Na hizo saba zipo Kwikonero,Hospitali ya Halmashauri, Masinono Kata ya Bugwema, Kurugee Kata ya Bukumi, Murangi Kata ya Murangi,Rusoli Kata ya Rusoli,Nyang’oma Kata ya Mugango na  Nyasurura Kata ya Ifulifu. 

Hata hivyo Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo alileta Ambulances tano kati ya hizo saba  zilizoko Jimboni humo.