February 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kituo cha afya Kisiwa cha Rukuba chafungiwa umeme jua kurahisisha huduma

Fresha Kinasa, TimesMajira Online Mara.

KITUO cha Afya cha Kisiwa cha Rukuba Kilichopo katika  Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mkoani Mara kimefungiwa umemejua (solar energy) wa thamani ya Shilingi  Mil. 345.6  ili kuimarisha utoaji wa huduma za matibabu kwa Wananchi wanaofika katika kituo hicho ambacho kimeanza kutoa matibabu.

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospter Muhongo Februari 23, 2025 kupitia taarifa yake kwa Wananchi ambapo pamoja na mambo mengine amesema kuwa Sehemu nyingine za Kisiwa hicho zitafungiwa umemejua (solar energy) kupitia Mradi mkubwa wa kufungia umemejua kwenye Visiwa vya nchi nzima vilivyoko Bahari ya Indi na Maziwa yetu makuu.

“Kwa hiyo, Kisiwa cha Rukuba nacho kiko ndani ya Mradi ambao matayarisho yake yanakamilishwa (Taarifa kutoka REA kwenda kwa Mbunge wa Jimbo)”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha Prof. Muhongo kupitia taarifa hiyo ameongeza kuwa, baada ya umemejua kusambazwa Kisiwani Rukuba, RUWASA itaendelea na mradi wake wa kusambaza maji ya bomba Kisiwani humo.

Kuhusu elimu kisiwani Rukuba amesema,  Kisiwa hicho  kina Shule ya Msingi yenye Maktaba na nyumba za makazi ya walimu wote. Na  upungufu wa vyumba vya madarasa haupo. Huku pia akisema  Sekondari mpya inajengwa Kisiwani humo, na imepangwa ifunguiliwe mwaka huu, 2025.

Wananchi wa Kisiwa cha Rukuba na Viongozi wao wa ngazi mbalimbali wameishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi  ya ya Kisiwa cha Rukuba

“Ninayo furaha kubwa kuona kituo cha Afya Rukuba  kimekuwa msaada kwetu kutuhudumia. Tukiugua hatupati shida kama hapo awali ambapo tulilazimika kusafiri kwa  kupanda boti kwenda Kutibiwa Musoma Mjini.” amesema Paulo Mathias.

Naye Neema Marwa amesema kuwa, uwepo wa kituo hicho kisiwani hapo,  kumesaidia kwa kiwango kikubwa Wananchi kuokoa gharama na muda mwingi ambao awali waliutumia kufuata matibabu katika Hospital zilizopo Mjini  Musoma na muda mwingi kushindwa kutumika kufanya shughuli za uzalishaji.

Wakazi wa Kisiwa hicho waliamua   kupanua Zahanati yao iwe Kituo cha Afya. Ambapo  upanuzi ulianza kutekelezwa kwa kutumia michango ya fedha na nguvu kazi za Wananchi na michango ya  Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini    Prof. Muhongo na Serikali pia ambayo ilitoa  Shilingi Mil. 500.