November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kitete: Kambi ya madaktari Bingwa yaanza upasuaji

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kambi maalumu ya Madaktari Bingwa kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Dodoma imeanza kufanya upasuaji kwa wagonjwa waliokutwa na uhitaji wa huduma hiyo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete.

Hayo yamesemwa leo na Kiongozi wa Madakatri hao ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Tumbi Dkt. Amani Malima ambapo zoezi hilo limeanza siku ya jumatatu na litadumu kwa siku tano.

Amesema kuwa kwa siku ya kwanza walianza kuwaona wagonjwa na kuweza kuwachambua na kwa wale waliohitaji upasuaji, wameanza huduma hiyo toka siku ya jumanne katika idara ya Mifupa, Masikio, Pua na Koo pamoja na matumbo.

“Jana tulifanya upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya Masikio, Koo na Pua pamoja na matumbo, kwahiyo leo tunaendelea kwa upande wa idara Mifupa hususani kwa watoto wenye matatizo ya mifupa ambayo wamezaliwa nayo, pia kuna watu waliopata ajali lakini wamekuwa na ulemavu ambao unaweza kurekebishika hivyo tupo hapa kwa nia ya kuwasahihisha”. Aliongeza Dkt. Malima.

Aidha, Dkt. Malima amesema lengo kubwa la kambi hiyo ni kutoa huduma za matibabu ya kibingwa wa wananchi wa mkoa wa Tabora na kuwapunguzia gharama za kuzifuata huduma hizo nje ya mkoa kwani wananchi wengi wamekuwa wakifuata huduma Dar es salaam, Mwanza, Kilimanjaro na Dodoma.

“Serikali yetu kupitia kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekua ikifanya vizuri na mambo makubwa katika sekta ya afya, hivi sasa kuna maboresho ya miundombinu yakiwemo majengo na ununuzi wa vifaa tiba hivyo tumewaleta madaktari mabingwa hawa ili kuweza kutoa huduma hizi kwa fani mbalimbali.

“Sisi kama wataalamu wa hospitali za rufaa za mikoa tumeona ni vyema kujiongeza licha ya kuwapunguzia gharama watanzania wa kuzifuata huduma hizi nje ya Tabora lakini tutawajengea pia uwezo wataalamu wa hospitali hii ili kuhakikisha wananchi wa hapa wanaendelea kupata huduma kama hizi, hivyo tumeuda kikundi cha madaktari bingwa kutoka fani mbalimbali zaidi ya ishirini”.

Hata hivyo Dkt. Malima amesema kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya uliofanyika kuanzia ngazi ya Zahanati, Vituo vya Afya, hospitali za wilaya na hospitali za rufaa za mikoa, hivyo amewataka wananchi kuhakikisha wanafika kupata huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na si kwingineko.

Dkt. Malima pia amewaomba wafanyabiashara, makampuni na watu wenye uwezo wajitokeze kusapoti huduma kama hizo kwenye maeneo yao waliyozaliwa ili kuweza kuwasaidia wananchi katika huduma za afya.

Naye, Mkazi wa Uyui Bi.Christina Lukwiza ambaye amemleta mtoto wake anayesumbuliwa na tatizo la kupumua kwa miaka minne sasa amesema alifurahi mara baada ya kusikia kuna madaktari bingwa kwenye hospitali ya Kitete.

“Nimeshazunguka kwenye hospitali mbalimbali na kuambiwa mwanangu ana vinyama kwenye pua na tumekuwa tukipewa dawa na kuzitumia ila tatizo halijaisha na hivyo kusababisha mahudhurio hafifu shuleni na wakati mwingine tunashindwa kumpeleka hospitali nyingine kwani hatuna uwezo wa kifedha”amesema Bi. Christina

Ameongeza kuwa amekimbilia hospitalini hapa kwakuwa hakuna gharama za kumuona daktari bingwa pia hata huduma zingine ni kuchangia kidogo.

“Nimekimbilia hapa ili mwanangu aonane na madaktari bingwa, kwani nilikua nawaza sana lini mwanangu ataonana na madakari bingwa, kwakweli ujio wao umenifurahisha sana kwani najua watatusaidia hasa sisi wenye kipato kidogo”.

Madaktari bingwa kutoka hospitali za rufaa za mikoa ya Dar es Salaam,Pwani na Dodoma wakifanya upasuaji kwa wagonjwa waliofika kupata matibabu katika kambi ya siku tano Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete.
Madaktari Bingwa wa Masikio,Koo na Pua wakifanya upasuaji kwenye kambi ya siku tano inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete.
Kiongozi wa Madaktari Bingwa ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Tumbi Dkt. Amani Malima akiongea kuhusu huduma za upasuaji na matibabu yanayofanyika katika kambi hiyo.
Wataaamu wakijiandaa na upasuaji katika kambi ya Madaktari Bingwa inayoendelea katika hospitali ya rufaa ya Kitete Mkoani Tabora.
Baadhi ya wakazi wa Tabora wakisubiri huduma za matibabu kutoka kwa Madaktari Bingwa katika idara mbalimbali