December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kitengo kipya cha majanga ya ajali kushughulika kuokoa maisha ya watu

Na Englibert Kayombo WAF – Dodoma.

Wizara ya Afya imeendelea kuboresha mikakati ya kuokoa maisha ya watu kutokana na majanga na ajali kwa kuanzisha Kitengo mahsusi kitakachoshughulika na kuokoa maisha ya watu kutokana na ajali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu leo akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alipowatembelea majeruhi wa ajali iliyohusisha Basi la Arusha Express kugongana na Lori eneo la Mzakwe, Dodoma.

“Katika Mipango yetu pale Wizarani, Kitengo cha Magonjwa yasiyoambukiza sasa hivi tutakiita Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza, Ajali na Afya ya Akili”. Amesema Waziri Ummy Mwalimu.

“Ajali zinatokea, lakini ni wajibu wetu ajali zinapotokea kuhakikisha tunatoa msaada wa haraka kwa majeruhi wa ajali, kwa hiyo hili ni eneo ambalo tutalipa kipaumbele”. Amesisitiza Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema pia katika Wizara ya Afya ipo Idara ya Utayari na Udhibiti wa Majanga na Magonjwa ya Mlipuko na kuwataka pia kutojikita kwenye kushughulikia magonjwa ya mlipuko pekee bali pia na kuwa na mwitikio wa haraka kushughulikia majeruhi wa ajali.

Waziri Ummy amesema kupitia Idara hiyo, vilianzishwa vituo vya utayari na dharura kushughulikia majanga na ajali pembezoni na barabara kuu kutoka Dar Es Salaam hadi Mbeya hivyo kuwataka watalaam kuwa na mpango huo kwa barabara ya kuelekea Mkoa wa Dodoma.

Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kuwapa pole majeruhi wote wa ajali hiyo na kuwatakia afya njema na kupona haraka pamoja na kuwapongeza watoa huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa kuwahuduma vyema wagonjwa na majeruhi wa ajali hiyo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest amesema Hospitali hiyo ilipokea majeruhi 22 pamoja na watu sita waliofariki ambapo kati ya majeruhi hao 1 alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Dkt. Ibenzi amesema katika majeruhi 21 waliokuwa katika Hospitali hiyo, 1 alifariki, watu 9 walipewa ruhusa na 11 wamesalia wakiendelea kupatiwa huduma za matibabu.