Na Jackline Martin, TimesMajira Online
KITENGO cha Afya ya Mama na Mtoto CCBRT -Samia Suluhu Hassan Maternity Wing kimepatiwa mashine ya Ultra Sound, ili kiweze kutatua changamoto zinazowakabili wakina mama wajawazito wanaoenda kupata huduma za afya katika Hospitali ya CCBRT, jijini Dar es Salaam.
Kitengo hicho kilizinduliwa Julai mwaka huu na Rais Samia kuitwa CCBRT Samia Suluhu Hassan Maternity Wing’ kikiwa na lengo la kuwahakikishia akina mama wote uzazi salama. Mashine hiyo ilitolewa na Kampuni ya Kuhudumia Mashirika ya Ndege, Abiria na Mizigo katika Viwanja vya Ndege (Swissport) ambapo ina thamani ya sh. milioni 68 ikilenga kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi sambamba
na kuzuia ulemavu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa makabidhiano ya mashine hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Swissport Tanzania, Mrisho Yassin alisema wanatambua changamoto ya
vifaa tiba ambayo ipo katika hospitali hiyo ya CCBRT, hivyo kifaa hicho kitasaidia sana jamii
ya Watanzania hasa akina mama wajawazito.
“ Tunatambuakuna changamoto ya vifaa tiba na sisi kama kampuni ikiwa ni sehemu ya mchango wetu katika jamii tumeweza kutoa mchango wetu huu wa Ultra Sound utakuwa unatumika hapa CCBRT,” alisema Mrisho na kuongeza;
“Kifaa hiki cha Ultra Sound kitasaidia sana kwa sababu ni mashine ambayo itakuwa inahitajika sana hapa CCBRT na sisi tunafurahi kwa sababu tunaamini mashine hii itatumika na mchango wetu katika jamii utatumika ipasavyo kusaidia jamii ya Watanzania ambao ni jamii ya akina mama wajawazito”
Kwa upandewake Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi alisema takribani asilimia 87 ya
wagonjwa wanaofika CCBRT kwa ajili ya kupata matibabu ni wagonjwa ambao aidha wanapata huduma za bure au wanachangia, hivyo ameziomba kampuni mbalimbali kuendelea kuwashika mkono katika maeneo mbalimbali ikiwemo huduma za kibingwa za afya na vifaa tiba ili waweze kuwasaidia akina mama hao wajawazito na watanzania wengine wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali yanayotibika.
“Sisi kama CCBRT tunahitaji kushikwa mkono kwenye eneo la huduma za kibingwa na bobezi za afya, namna ambavyo tumeendelea kuwapa mafunzo wafanyakazi wetu yaani watoa huduma na vifaa na vifaa tiba”
Aidha, Msangi alisema tangu kuanza kutolewa kwa huduma katika kitengo cha mama na mtoto Januari hadi Oktoba 2022 wameweza kuhudumia akina 225.
Mbali na hayo, Msangi aliwataka akina mama wajawazito walioko katika kundi maalumu na wengine wote, kuhudhuria kliniki mara wanapojigundua kuwa wajawazito ili kuweza kufuatiliwa maendeleo ya afya zao.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini