November 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kitandula afanya ziara TAWIRI

Na Queen Lema, Timesmajira Online, Arusha

Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ina mchango mkubwa sana katika sekta ya uhifadhi wa malisili na uboreshaji wa biashara ya utalii nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dunstan Kitandula (Mb) wakati akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi na Menejimenti ya TAWIRI, Dkt.Kitundula alipotembelea ofisi za Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti Wa Wanyamapori Tanzania(TAWIRI) zilizopo Njiro, Jijini Arusha.

Mhe. Kitandula alisema kuwa , tafiti za TAWIRI zinamchango mkubwa katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini, ambapo amewapongeza wataalamu wa TAWIRI kwa umahiri na ubobevu, ambao umewaleta wadau kutoka nchi mbalimbali kuja kupata uzoefu kama vile sensa za wanyamapori.

“niwapongeze kwa umahiri wenu, kwani mnashiriki kukuza utalii kupitia zao jipya la utalii wa utafiti ” amepongeza Dkt. Kitandula.

Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi TAWIRI, Dkt.David Manyanza amesema bodi hiyo na wataalam kupitia mpango mkakati utakaohuishwa imeandaa vipaumbele vitakavyoongeza wigo wa Taasisi hiyo kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kisayansi kwa wakati ili kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii nchini.

Awali,akitoa taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI Dkt. Eblate Ernest Mjingo amesema mbali na taasisi hiyo kuwa na wataalam mahiri, inatumia teknolojia za kisasa katika tafiti ikiwa ni matumizi ya visukuma mawimbi kuwafuatilia wanyamapori, matumizi ya akili mnemba (artificial intelligence) kufanya sensa ya wanyama.