December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kitalu nyumba kuleta matokeo chanya uzalishaji mazao

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

CHUO Kikuu cha Dodoma ( UDOM),kimefanya utafiti na kubaini teknolojia ya kitalu nyumba inaleta matokeo chanya kwa mazao ya mbogamboga mkoani Dodoma

Kufuatia hali hiyo amewaasa wananchi walime kisasa kwa kutumia njia ya kitalu nyumba ili kupata mazao bora na kuongeza tija katika kilimo ,uchumi wao na Taifa kwa ujumla

Mtaalam wa Maabara wa UDOM , Julius Ngumba amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji yanayoendelea Jijini Dodoma.

Amesema kwa kutumia teknolojia hiyo wameweza kulima mazao hayo ya mboga mboga kama nyanya, matango, karoti na hoho,wameotesha na miti ambapo vyote vinastawi vizuri.

“Dodoma kuna uhitaji mkubwa wa vyakula lakini ni eneo ambalo jamii yake ina udumavu unaochangiwa na upungufu wa virutubisho katika jamii.

“Mboga zilikuwa haba kutokana na uhaba wa maji lakini utumiaji wa Green House (kitalu nyumba )’unatatua changamoto hiyo,” amesema.

Amesema kwa kutumia teknolojia hiyo mazao ya mboga mboga yameweza kufanya vizuri huku akisema jamii ya mkoa huo ikiamua kuachana na kilimo cha asili walichokizoea wataweza kuzalisha mazao bora kwa msimu wote kwa mwaka mzima.

Amesema ” kuhama njia asili kwenda mpya kuna gharama. Wakiweza kujenga watazalisha mazao bora msimu wote wa mwaka,”amesisitiza mtaalam huyo