December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kipanga aitaka jamii kuitumia TAEC kwa ajili ya kunufaika na Mionzi

Na Penina Malundo

NAIBU Waziri Wizara wa Elimu, Sayansi na Tekonilojia, Omary Kipanga ameitaka jamii kuitumia Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kwa ajili ya kunufaika na bidhaa na utaalamu wa aina tofauti ikiwemo masuala ya mionzi.

Naibu Waziri Kipanga amesemwa hayo juzi alipotembelea banda la TAEC katika maonesho ya 47 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Temeke jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa tume hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuratibiwa na kuthibiti mionzi ili isiweze kuleta athari kwa wananchi na kwamba matumizi ya mionzi yana wigo mpana katika masuala ya matibabu na tafiti kuhusu namna ya kuweza kuhifadhi vyakula kwa kutumia mionzi hiyo.

“Watanzania tukitumie kituo chetu hiki cha TAEC ili tuweze kunufaika Zaidi na bidhaa pamoja na utaalamu wa aina tofauti ambao wanautoa hasa katika masuala mazima ya mionzi, hatuwezi kuagiza chakula kutoka nje au kukitoa bila kuhakikisha kama kipo salama kwa upande wa mionzi na matumizi ya binadamu,”amesema na kuongeza

“Tunafahamu pia ukienda hospitali, tunatumia mionzi kwa ajili ya matibabu kama ukitaka kupigwa X-ray na ultrasound, ST SCAN. Kazi inayofanywa na tume hii ni kubwa bahati nzuri nimepata fursa ya kutembelea pale Arusha na kuona namna gani mionzi inaweza kuratibiwa, kuthibitiwa ili isiweze kuleta athari kwa wanaadamu,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Lazaro Busagala amesema majukumu ya tume hiyo ni kuhakikisha watanzania wanakuwa salama na wasije wakadhurika na hatari ambayo inaweza kusababishwa na mionzi.

Busagala ametoa wito kwa wananchi kuitumia tume hiyo na kubainsiha kuwa kwa sasa wanazo ofisi zisizopungua 52 nchi nzima hivyo wananchi hao wanaweza kupata huduma zao karibu zaidi walipo.