Na Mwandishi Wetu,Timesmajira. Online, Hai
WANANCHI katika Kata ya Longoi wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro, wameeleza kusikitishwa na kutowekwa jiwe la msingi wa Zahanati ya Longoi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Maalumu wa Uhuru 2021, Luteni Josephine Mwambashi kwa kile kilicholezwa na kukosekana kwa nyaraka zinazoonesha matumizi ya fedha zilivyotumika.
Dauson Mushi mkazi wa kata hiyo, amesema walikuwa na matarajio makubwa zahanati yao kuzinduliwa kwa kuwekwa jiwe la msingi, lakini mambo yamekuwa ni kinyume jambo linalowakatisha tamaa katika kuchangia miradi ya maendeleo.
Naye Doris Mollel mkazi wa kata hiyo, amesema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakipata adha ya kwenda umbali mrefu kupatiwa matibabu na anaamini, kama kuna watu walioshiriki kuhujumu zahanati hiyo wataenda kuchukuliwa hatua.
Kwa upande wake Kiongozi huyo wa Mwenge Maalumu, Luteni Mwambashi amekataa kuweka jiwe la msingi katika zahanati hiyo kwa kile alichokieleza kuwa hakuna nyaraka zinazoonesha mtiririko wa utoaji fedha pamoja na matumizi.
Hata hivyo ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Hai, kuchunguza mtiririko mzima wa fedha zilizochangwa kwa ajimi ya ujenzi wa zahanati hiyo na matumizi yake, yalivyokwenda na kuagiza apatiwe ripoti hiyo mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge Maalumu ameridhishwa na miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo imetekelezwa wilayani hapa, ikiwemo mradi wa kusambaza maji kutokana chanzo cha MusaToroka ambapo zaidi ya sh. milioni 400 zilizotumika zimetokana na Serikali Kuu.
Miradi mingine ni barabara ya lami kutoka TTCL hadi Katoliki ambapo zaidi ya sh. milioni 355, zimetumika kwa ajili ya ujenzi huo ambao utarahisisha wananchi wanaokwenda kupata huduma katika Hosipitali ya Wilaya.
Riziki Lesuya ambaye Ofisa Uhusiano Wilaya ya Hai, akimweleza Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge amesema kituo cha Redio cha Boma Hai, kimepewa ruzuku ya sh. milioni 40 kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO na hivyo kuwezesha radio hiyo, kutoa huduma za upashanaji wa habari kwa maendeleo ya wilaya hiyo.
“Kauli ya Mbio za Mwenge ni kuhusu matumizi sahihi ya TEHAMA kwa maendeleo na hapa leo (juzi), kiongozi unaweza kujionea kwa vitendo namna ambavyo sisi watu wa Hai, tulishatangulia katika kuleta maendeleo kwa kutumia na hata hii ruzuku tuliyoipata imetuongezea wigo wa utoaji habari,” amesema.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea