Na Mwandishi wetu, timesmajira, Dar es Salaam
Kiongozi Mkuu wa madhehebu ya Kiislamu ya Mabohora (Dawoodi Bohoras); Sheikh Syedna Mufaddal Saifuddin, ametua nchini leo Alhamisi Juni 16, 2022, tayari kufanya ziara ya kiimani na mapumziko mafupi.
Saydna Mufaddal, atakuwa nchini kwa takribani wiki mbili ambapo pamoja na shughuli za kiimani amekuja kuunga mkono azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza na kuifungua nchi hasa kupitia filamu ya Royal Tour.
“Hapa nchini amekuja kuunga mkono malengo ya Royal Tour na yeye mwenyewe na wafuasi wake watakwenda mapumziko na msafara wake wote katika maeneo mbalimbali na pia iwapo taratibu zitakamilika na akaridhia anaweza kufanya mhadhara wake mkubwa wa kidini Julai hapa nchini ambapo wafuasi wake kati ya 30,000 hadi 40,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani humfuata na tunajipanga ikitokea hivyo tutawaonesha watu hao na mabohora wengine duniani filamu ya Royal Tour,” amesema mmoja wa viongozi wa dhehebu hilo nchini Zainuldeen Adamjee.
Akimpokea Kiongozi huyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema amewasilisha kwa kiongozi huyo salaam za Mhe Rais Samia ikiwemo utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mhadhara mkubwa wa mwaka wa kiongozi huyo utakaoleta maelfu ya watu hapa nchini.
“Hii ni sehemu ya muendelezo wa Royal Tour (post royal tour) ambapo Rais wetu amefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi yetu na sasa wawekezaji na watalii wakiwemo viongozi wa kimataifa wa kiimani na wa kijamii nao wanazidi kuja Tanzania. Kwa eneo letu sisi la utamaduni tumemhakikishia Sheikh kuwa Tanzania ni salama na aendelee kutuombea amani lakini pia alete wafuasi wake wengi zaidi kuja kutembelea na kuwekeza Tanzania,” amesema Waziri Mchengerwa.
Katika mapokezi hayo, Waziri Mchengerwa, aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, ambaye pia anasimamia Kamati ya Rais iliyoratibu Royal Tour.
More Stories
Mwinyi: Kuna ongezeko la wawekezaji Zanzibar
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi