January 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kinana apewa heshima ya Utemi wa wanyamwezi

Na Allan Vicent , TimesMajira Online

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Komredi Abdulrahman Omari Kinana amehitimisha ziara yake Mkoani hapa kwa kuvishwa vazi rasmi la Utemi wa Wanyamwezi na kupewa jina la Mtemi Kiungi.

Kinana amepewa heshima hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Chipukizi, katika halmashauri ya manispaa Tabora na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Viongozi na wanachama wa CCM na vyama rafiki.

Akizungumza katika mkutano huo Komredi Kinana alisema wanaCCM, Viongozi na watendaji wote wa serikali wataendelea kumsifia Rais Dkt Samia kwa kuwa anafanya kazi nzuri sana ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema tangu aingie madarakani mapato ya ndani yamevunja rekodi na ameweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji kodi pasipo kutumia nguvu kwa walipa kodi, amejenga mahusiano mazuri na mataifa mbalimbali ikiwemo taasisi za kimataifa na zimeendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi .

Aidha Kinana alimpongeza Rais Samia kwa kuongoza nchi katika misingi ya amani ikiwemo kutoa uhuru kwa wanasiasa kufanya mikutano ya hadhara, huku akiwataka kutumia uhuru huo vizuri na sio kukujeli au kumtukana Rais.

‘Rais Samia ni mzalendo namba moja, anajali wananchi wake wote, hana kinyongo na mtu yeyote, wale wanaokosoa au kukejeli utendaji wake punguzeni jazba, matusi, kejeli na dharau havisaidii chochote’, alisema.

Kinana alibainisha kuwa Rais hana kinyongo na wapinzani ndiyo maana amewaruhusu kufanya mikutano ila akawataka kuwa waungwana na kujenga hoja zenye mashiko kwa jamii na sio kuendeleza kejeli, dharau na matusi kwa kuwa hayatawasaidia.

Awali akimkaribisha katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassaan Wakasuvi aliipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kusimamia utekelezaji ilani ya uchaguzi kwa asilimia 100.

Alisema CCM inajivunia kuwa na Rais mchapakazi, msikivu, anayejali maslahi ya wananchi, asiyependa makuu na anayejitoa wakati wote kusaidia wananchi wake, aidha alimpongeza Makamu Mwenyekiti kwa kuendelea kuimarisha chama hicho.