Na Penina Malundo,Timesmajira
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu. Kimbunga “HIDAYA” kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi ya Tanzania.
Taarifa iliyotolewa leo na TMA,imesema hadi kufika saa tatu usiku ya tarehe 02 Mei 2024 kilikuwa umbali wa takriban Kilomita 402 Mashariki mwa pwani ya Mtwara.
Imesema nguvu ya kimbunga HIDAYA imeendelea kuimarika na kuwa kubwa zaidi, ambapo hadi kufikia usiku huu kasi ya upepo katika kimbunga imeimarika na kufika Kilomita 110 kwa saa na inatarajiwa kuendelea kuimarika zaidi katika kipindi cha saa 24 zijazo.
“Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga “HIDAYA” kuendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania na kuendelea kuwepo hadi tarehe 06 mwezi Mei 2024. Hata hivyo, kimbunga hicho kinatarajiwa kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024,”imesema.
Aidha imeeleza uwepo wa kimbunga “HIDAYA” karibu na pwani ya nchi ya Tanzania ,unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani. “Vipindi vya mvua nyepesi na upepo wa wastani tayari vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Mtwara. Ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 Mei 2024,”imesisitiza na kuongeza
“Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza,”imesema.
Pia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba