March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilombero sugar yazindua mpango wa Tehama mashuleni

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Sukari Kilombero imezindua rasmi Mpango wa Uwezeshaji wa TEHAMA Mashuleni, mradi wa kijamii unaolenga kuzipatia shule za sekondari vifaa na ujuzi wa kidijitali, huku ukiwanufaisha zaidi ya wanafunzi 1,000 katika Bonde la Kilombero.

Kupitia mpango huo, Kilombero Sugar imetoa kompyuta 35 za mezani na meza 10, pamoja na msaada wa kiufundi kutoka kitengo chake cha TEHAMA, kwa Shule ya Sekondari Nyange (Wilaya ya Kilombero) na Shule ya Sekondari Lyahila (Wilaya ya Kilosa).

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Kampuni hiyo, Diana Mwakitwange, amesema mpango huo unaendana na vipaumbele vya kitaifa ikiwemo Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Kidijitali 2024/25–2029/30 na Mwongozo wa Taifa wa Akili Bandia kwa Elimu, unaolenga kubadilisha mfumo wa elimu nchini.

Kwa upande wake,Victor Byemelwa, Meneja Mawasiliano na Mahusiano ya Wadau, alieleza kuwa shule zilizochaguliwa zilitathminiwa kwa vigezo maalumu ikiwemo uwepo wa mwalimu wa TEHAMA, chumba cha kompyuta na utayari wa kutekeleza ajenda ya elimu ya kidijitali. Alibainisha pia kuwa mpango huo ni endelevu na utatekelezwa kwa awamu.

Akizungumza kama mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero,Wakili Dunstan Kyobya, alisifu hatua hiyo na kueleza kuwa serikali inaendelea kuimarisha uwezo wa walimu na watendaji wa elimu katika matumizi ya zana za kidijitali.

Amewataka wadau wengine kuunga mkono juhudi hizo ili kuchochea mageuzi ya elimu.Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyange, Bw. Gabriel Lyaluu, alishukuru msaada huo akisema umefika wakati muafaka, huku Amina Ally, mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Lyahila, akieleza furaha yake kwa kupata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu TEHAMA.

Mpango huu unatarajiwa kuendelea kupanuka kwa shule nyingine ndani ya Bonde la Kilombero, ukichochea mageuzi ya elimu ya kidijitali nchini Tanzania.