November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilombero Sugar Yazindua Kampeni ya ushirikishaji Wakulima na uwekezaji

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kampuni ya Kilombero Sugar imezindua kampeni ya Ushirikishaji wakulima na uwekezaji kama sehemu ya Mradi wake wa Kupanua kiwanda cha K4.

Hadi sasa mradi huo umefikia 90%, ambapo wakulima wataweza kuzalisha 60% ya miwa inayohitajika katika kiwanda hicho.

Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi uliofanyika katika mashamba ya miwa ya Kilombero ambayo imehudhuriwa na watu mbalimbali, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bw. Dunstan Kyobya, amepongeza juhudi za Kilombero Sugar kwa Uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo itaenda kuinua kipato endelevu kitakachoboresha maisha ya wakulima wa miwani.

“Mpango huu wa Kupanua kiwanda cha K4 na kampeni ya Kuinua Wakulima ni jambo muhimu kwa kipato endelevu kitakachoboresha maisha ya wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero,” alisema Bw. Kyobya. “Serikali imejitolea kuunda mazingira mazuri kwa uwekezaji wa biashara na ustawi wa jamii.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wakulima wa nje Kilombero Sugar, Pierre Redinger akisisitiza jukumu muhimu la jamii katika jitihada hizi , amesema uwekezaji huo unatokana na imani waliyonayo kwa wakulima wao.

“Uwekezaji wetu katika Mradi wa Kupanua kiwanda cha K4 unatokana na imani tuliyonayo kwa wakulima wetu, Safari hii ilianza mwaka 2018 kwa usajili wa wakulima, ukiungwa mkono na Ofisi ya Wilaya ya Kilombero, ambao ulifungua njia kwa biashara hii muhimu.”

Mbali na hayo, Redinger amesema kuwa Kampuni hiyo imejitolea kutoa mkopo wa mbegu za miwa tani 20000 kwa wakulima, kwa msimu wa upandaji wa 2024/25 na 2025/26, ambao utasaidia zaidi upanuzi huo.

Naye George Gowelle, ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, ameelezea mchango mkubwa wa serikali katika mradi huo, akisema kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kuongeza utoshelevu wa sukari.

Ameongeza kuwa. “Kilombero Sugar imeweka mfano wa kuigwa, na serikali itaendelea kuunga mkono jitihada kama hizi.”

Mwenyekiti wa Kilombero Joint Enterprises Cooperatives Society, inayowakilisha AMCOS 17 zinazofanya kazi moja kwa moja na Kilombero Sugar, Bakari Mkangama, ameisifu kampeni hiyo kama fursa ya mabadiliko.

“Mpango huu utaleta mabadiliko makubwa kwa soko letu la kuaminika, kipato endelevu, na kuboresha maisha,” alisema Bw. Mkangama. “Tunapaswa kuchangamkia fursa hii adhimu.”

Kampeni hiyo imeenda sambamba na Wenye kaulimbiu ya ‘Soko la kuaminika, kipato endelevu, na kuboresha maisha’ ambayo inalenga kuimarisha maendeleo miongoni mwa wakulima wa miwa kupitia mawasiliano ya kimkakati na ushirikiano na wadau.