November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilio cha riba za mabenki kwa wakulima wa Mkonge kupata ufumbuzi

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imesikia kilio cha suala la riba kubwa inayotolewa na benki za biashara kwa wakulima wa Mkonge ambapo tayari benki kuu ya Tanzania imetoa tamko la kuzitaka benki hizo za biashara kutotoza riba ya zaidi ya asilimia 10 kwa mikopo ya kilimo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri wa Kilimo Antony Mavunde kwa niaba ya Waziri mkuu Majaliwa katika Mkutano wa tatu wa wadau wa Sekta ya Mkonge Tanzania uliyofanyika Jijini Tanga uliokwenda sambamba na kauli mbiu ya Mkonge ni Biashara Wekeza Sasa.

Waziri Majaliwa amesema suala la riba kubwa iliyokuwa ikitozwa na mabenki ya biashara kwa wakulima wa Mkonge ilikuwa ikiwafanya wakulima washindwe kufanya kilimo chao kwa ufanisi unaotakiwa wakihofia riba kubwa wanazotozwa.

Waziri Mkuu Majaliwa amezishukuru baadhi ya benki zilizoitikia wito huo ambapo nyingi zinatoza riba kwa mikopo ya kilimo kwa wastani wa asilimia 9.

“Niwasihi wakulima wa Mkonge kuimarisha kilimo hichi cha mkonge hususani kwa wakulima wadogo na wahamasishwe kujiunga katika vyama vya ushirika ili wapate mikopo na masoko ya kuuzia mazao yao, alisisitiza Naibu waziri Mavunde kwa niaba ya Waziri Mkuu.

Katika Mkutano huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameombwa kulichukua suala la makundi yaTembo kuvamia mashamba ya Mkonge na kuharibu mazao lipatiwe ufumbuzi kutokana na kwamba linawarudisha nyuma juhudi za wakulima wadogo ikiwemo kuwakatisha tamaa wakulima wa Mkonge.

Ombi hilo limetolewa na Mbunge wa jimbo Mkinga Dastan Kitandula wakati akitoa salamu zake kwenye mkutano huo ambapo amesema kuwa pamoja na Serikali kuweka msukumo kwa wakulima wadogo kujiingiza kwenye kulima zao hilo kinyume na ilivyokuwa zamani lakini kutokana na uwepo wa changamoto hiyo imekuwa ikiwashusha hari wakulima wa zao hilo.

Kitandula amesema licha ya kufurahishwa na jinsi Serikali inavyojielekeza kufufua zao la Mkonge na jitihada zinazofanyika na msukumo unaowekwa kwa wakulima wadogo wajiingize kwenye kulima zao hilo tofauti na ilivyokuwa siku za kinyume na hadi kuonekana kuwa zao wakulima wakubwa ambapo kwasasa mwako umekuwa mkubwa hasa kwa wakulima wadogo.

“Lakini lipo jambo ambalo Serikali inabidi ilichukulie kwa umuhimu mkubwa ili lisiwakatishe tamaa wakulima wa zao hilo hasa changamoto ya makundi ya Tembo kuvamia mashamba ya Mkonge”Alisema

“Hii ni changamoto kubwa sana na tumejitahidi kusema serikalini bado ni changamoto hivyo tunaomba mh Waziri Mkuu ulichukue ukazungumze na wenzako kwamba muone namna kudhibiti Tembo ili wasituulie zao la Mkonge pamoa na mengine” Alisema Mbunge Kitandula.

Hata hivyo Mbunge huyo alisema tamaa yao vilevile ni kuona wakati jitihada za kufufua zao wajielekeze kwenye maeneo mengine wataongeza thamani ya zao hilo ili kutengeza fedha ili Utafiti ifanyike tuweze kupata mafanikio zaidi kwenye zao hilo.