July 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kikwete atoboa siri mafanikio CCM uongozi wa Rais Dkt, Samia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, amesema anafurahishwa na namna makada, wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi wa RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanavyoendeleza umoja miongoni mwao.

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, amesema umoja miongoni mwa wanachama ndio nguzo na silaha muhimu hasa wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Kiongozi huyo mstaafu amesema hayo jana Julai 1, 2024, alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi aliyemtembelea kumjulia hali kwenye ofisi yake binafsi, jijini Dar Es Salaam.

Rais Mstaafu Kikwete ametumia nafasi hiyo kumwambia Balozi Nchimbi kwa jinsi anavyofurahishwa na namna maelekezo anayotoa Mwenyekiti wa CCM, Dkt Samia Hassan ya kuwataka viongozi wa Chama kushuka chini kwa wanachama na wananchi kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua kero zao, yanavyotekelezwa kikamilifu.

Aidha, Rais Kikwete ameipongeza sekreterieti mpya ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa jinsi inavyojikita katika kuimarisha chama na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya 2020 -2025 kwa wananchi.

“Umoja na mshikamano wa wana-CCM ndiyo umekuwa siri na silaha ya ushindi wa CCM, ndiyo maana tunasema siku zote umoja wetu ndiyo ushindi wetu.

Tunafurahia sana tunavyoona wana-CCM chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM , Rais Sama. Hongereni sana,” alisema Kikwete.

Kwa upande wake, Balozi Nchimbi amewashukuru viongozi wastaafu wa Chama na Serikali kwa jinsi wanavyofanya kazi ya kuwalea kiuongozi na kimaadili viongozi wa sasa.

Balozi Nchimbi alisema CCM itaendeleza utamaduni wa kuwaenzi na kuwasikiliza viongozi wastaafu.

Balozi Nchimbi alisema kwa uzoefu wa uongozi na kazi nzuri ya kulitumikia taifa waliofanya wakati wa uongozi wao, viongozi hao ni hazina kubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.