Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DODOMA
RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Nne na Mwenyekiti wa Mfuko wa Ushirika wa Wafadhili wa Elimu Duniani (GPE) Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mitaala ili kukidhi mahitaji ya soko Kitaifa na Kimataifa.
Kikwete ametoa pongezi hizo Juni 27, 2023 jijini Dodoma katika kikao na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kumpitisha kwenye kwenye Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo mwaka 2014 Toleo la 2023 na Mabadiliko ya mitaala.
Akizungumza katika kikao hicho pia ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutekeleza agizo hilo na kuwataka kuhakikisha mabadiliko ya mitaala yanaakisi Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Dunia kwa kutoa elimu bora kwa wote pamoja na kuhakikisha ubora wa wahitimu katika ngazi zote.
“Mageuzi haya ni ya msingi, ninaomba tuzingatie sana suala la ubora. Na katika utekelezaji hakikisheni umma wa watanzania unaelimishwa, mueleze kuhusu manufaa yake sasa na hata baadae” alisema Mhe. Kikwete
Kikwete ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali za kutekeleza mageuzi hayo kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amemshukuru Mhe. Kikwete kwa kukubaki kushiriki katika kikao hicho na kutoa maoni kuhusu muelekeo huo mpya wa Sera ya elimu na Mitaala.
” tinakushukuru sana kwa maoni na nia yetu ni kuhakikisha tunapoanza utekelezaji hasa upande wa Amali tunaanza kwa ubora wa hali ya juu, ndio maana tunahitaji sana ushiriki wa wadau” , amesema Prof.Mkenda.
Aidha Prof. Mkenda amemhakikishia kuwa Wizara imejipanga kikamilifu katika kutekeleza kwa awamu malengo yote ya Sera baada ya kupitishwa Rasimu hiyo kulingana na ratiba inavyopendekeza.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja