Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dodoma
WAKATI Serikali ikiongeza jitihada za kupambana na ugonjwa wa UVIKO 19 , kikundi cha Wana-Makutu (Programu ya Chama) ambacho kinawajumuisha washiriki wa mafunzo ya kwa mujibu wa sheria waliofanya mafunzo mwaka 1989/1990 katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Kikosi 834 KJ Makutupora wameunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo na kupambana na ugonjwa huo kwa kuwezesha ununuzi wa vifaa tiba na kuvigawa katika hospitali kuu ya Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa tiba hivyo, Mwenyekeiti wa Wana-Makutu, Mhandisi Phillip Makota alisema kutokana na umuhimu wa vifaa tiba hivyo, Wana-Makutu wameamua kuunga mkono juhudi za Serikali dhidi ugonjwa wa Uviko-19 kwa kuchangia vifaa tiba vyenye thamani zaidi ya sh. milioni sita ikiwemo makasha ya barakoa, makasha ya vitakasa mikono na makasha ya gloves.
“Kutokana na utaratibu mzuri tuliojiwekea tulifanikiwa kukusanya fedha kutoka kwa wana-makutu na tumeona eneo kubwa la kuanza nalo ni hili la kununa vifaa tiba hivi vitakavyosaidia kwenye jitihada za kupambana na janga hili,” alisema mhandisi Makota.
Mhandisi Makota alimshukuru pia Mkuu wa Mkoa wa huo, Anthony Mtaka kutokana na ofisi yake kuratibu ziara nzima ya kikundi hicho ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuleta matokeo chanya.
“Kipeke ninapenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya wanakikundi kumshukuru Mkuu wetu wa Mkoa, Anthony Mtaka kwa kutusaidia kuratibu ziara hiyo na kuwa bega kwa bega na sisi mpaka tumefanikisha azma yetu,” alisema.
Awali kikundi hicho pia, kilipata fursa ya kutoa zawadi ya mabomba ya maji, zilizohusisha yenye kipenyo cha 16mm yenye urefu wa mita 4000 zitakazotumika katika umwagiliaji kwenye mashamba katika kikosi cha Jeshi cha 834 KJ Makotopora.
“Vifaa hivi kwa kiasi kikubwa vitasaidia katika ufanisi kwenye kilimo cha umwagiliaji kwenye bustani kutoka kumwagilia ekari 5 hadi kufikia ekari 7.5 jambo ambalo litaleta tija kwenye kilimo”, alieleza Mhandisi Makota.
Mhandisi Makota alitumia fursa hiyo kuwaomba wazazi kutowazuia watoto kwenye mafunzo JKT ya mujibu wa sheria kwa kuwa mafunzo hayo yanawajenga vijana wengi katika nidhamu, ukakamavu, uchapakazi, uzalendo na utayari kuwa askari wa akiba.
“Mimi nachukua nafasi hii kutoa rai kwa wazazi wenzangu kuwaruhusu watoto kujiunga na haya mafunzo ya jkt kwa mujibu wa sheria kwa kuwa mafunzo haya yatawajenga vyema kuwa wenye nidhamu, uzaledo, ukakamavu mkubwa kulitumikia Taifa pindi watakopoajiriwa”.alisema.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Hospitali,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Baraka Mponda,mbali ya kuwashukuru wana-Makutu, alisema msaada huo umefika wakati mwafaka kwani utasaidia sana kudhibiti maambukizi ya Uviko-19.
“Hii ni zawadi kubwa sana kutoka kwa vikundi vya wazalendo binafsi kwa mwaka 2021,” amesema na kuomba vikundi vingine kuiga mfano wa Wana-Makutu.
Kikundi cha Wana-Makutu kilianzishwa miaka 31 iliyopita kikiwahusisha vijana waliopita mafunzo ya jkt kwa mujibu wa sheria mwaka 1989/1990 ambapo lengo la uanzishwaji wake ni kushirikiana katika mambo ya kijamii huku mpaka hivi sasa kikundi hiki kinaratibiwa kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp ambapo mpaka sasa kinawashiriki wapatao 94.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua