Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Benki ya CRD leo imetangaza matokeo ya mauzo ya hatifungani yake ya kijani “Kijani Bond” ambayo imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 171.82 sawa na asilimia 429.55 ikilinganishwa na lengo la kupata shilingi bilioni 40 zilizopangwa awali.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamaja. Dkt. Mwamaja ameipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio hayo kwani fedha zilizokusanywa zitasaidia kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo na yenye faida nyingi za kimazingira kwa wananchi na taifa kwa ujumla, kutoa ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameelezea kuwa matokeo haya ni kiashirio cha imani walionayo wawekezaji wa ndani pamoja na nje ya nchi. Aidha, Nsekela alieleza kuwa asilimia 99 ya uwekezaji wa Kijani Bond unatokana na wawekezaji wa ndani, huku Shilingi bilioni 140 zikiwa ni fedha mpya katika mzunguuko jambo ambalo litachochea kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.
Kwa pamoja Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemas Mkama, na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mary Miniwasa wamesema haya ni mafanikio makubwa katika masoko ya mitaji nchini. Mniwasa amesema kuorodheshwa kwa Kijani DSE kutakwenda kuongeza uuzaji na ununuaji wa dhamana katika soko hilo maradufu kutoka wastani Shilingi bilioni 150 hivi sasa.
Tukio la kutangaza matokeo ya Kijani Bond lilienda sambamba na urodheshwaji katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ambalo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwamo Mkuu wa Idara ya Uchumi Ubalozi wa Uingereza, Euan Davidson, Mwakilishi Mkazi wa IFC nchini, Jes Chonzi, pamoja na wawekezaji na washirika mbalimbali wa Benki ya CRDB.
Kijani Bond ni toleo la kwanza la mpango wa miaka mitano wa Dola za Marekani Milioni 300 unaolenga katika kusanya fedha kwa ajili ya kufadhili miradi ya kijani, pamoja na miradi kijamii na endelevu.
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika