December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kijana auwawa na mamba akioga ziwani

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Nkasi

KIJANA mmoja aliyefahamika Kwa jina la Credo Yusiasi Siwale (16) mkazi wa Kijiji Cha Udachi kata ya Kabwe wilayani Nkasi Mkoani Rukwa amefariki baada ya kukamatwa na Mamba ziwa Tanganyika alipokuwa amekwenda kuoga.

Akizungumzia tukio Hilo Mwenyekiti wa Kijiji Cha Udachi Samwel Mwendapole amedai kuwa tukio Hilo limetokea Jana Jumatatu majira ya saa 5 asubuhi ambapo kijana huyo alikwenda kuoga ziwani baada ya kutoka shamba na Mama yake.

Amesema kuwa kijana huyo akiwa na mwenzie walikwenda kuoga ziwani na marehemu ndiye aliyetangulia kuingia majini na alipoingia tu alikamatwa na Mamba huyo na kutoweka naye kwenye maji mengi zaidi.

Amedai kuwa mwenzie baada ya kutoa taarifa hiyo serikali ya Kijiji ilipiga mbiu ya hatari na kuwataka Watu wote kujitosa majini kwenda kumsaka Mamba huyo.

Amefanya kuwa zoezi la kumsaka Mamba huyo liliendelea baada ya Watu WA Kijiji hicho kujitosa majini kuanzia muda wa saa 5 asubuhi walifanikiwa kuukuta mwili wa kijana huyo majira ya saa 8 mchana akiwa amekufa na kuhifadhiwa kwenye pango la mawe ndani ya ziwa Tanganyika.

Afisa mtendaji wa kata ya Kabwe Filbert Kwimba amethibitisha kutokea Kwa tukio Hilo na kusifu jitihada za Wananchi wa Kijiji hicho Cha kuamua kujitosa majini kwenda kukabiliana na Mamba huyo Ili kuweza kuokoa uhai wa kijana huyo.

Alidai kuwa Mamba baada ya kuona umati mkubwa wa watu wakimsaka aliamua kwenda kuuficha mwili wa kijana huyo kwenye pango na yeye kukimbia kuepuka hasira za Wananchi walipokuwa wakimsaka.

Kwimba pia aliwataka wakazi WA Kabwe kuendelea kuchukua tahadhari juu ya Mamba katika ziwa Hilo Kwani ni katika siku za hivi karibuni Binti mmoja alikamatwa na Mamba katika eneo Hilo Hilo na ambaye mwili wake haujapatikana hadi leo.

Afisa maliasili halmashauri ya wilaya Nkasi Valeriana Mwapasi amedai kuwa Hana taarifa juu ya tukio Hilo hivyo awezi kuzungumzia lolote.

Juu ya suala la kuwawinda Mamba hao amedai kuwa ofisi yake Kwa sasa ofisi yake Ina changamoto kubwa ya watumishi ambapo askari wengi wamestaafu na sasa askari ni mmoja na kuifanya kazi Yao kuwa ngumu.

Amedai kuwa lakini changamoto inapokuwa kubwa wao ushirikiana na askari wa TAWA pale inapotakiwa kwenda kuwawinda linapotokea tishio.
Mwisho