October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kijana aliyefungwa miaka 2 kwa kuchoma moto picha ya Rais aachiwa huru

Na Esther Macha TimesmajiraOnline, Mbeya

ALIYEFUNGWA miaka (2)kwa kuchoma moto picha ya Rais Samia, Shadrack Chaula (24) mkazi wa Kijiji cha Ntokela Kata ya Ndanto wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ameachiwa huru baada ya kulipa faini ya sh. Mil .5 ambazo amechangiwa na watu wananchi pamoja na wanaharakati kutoka maeneo mbalimbali.

Baada ya kutoka gerezani Shadrack Chaula amewashukuru wananchi wote kwa kuungana naye na kumsaidia kuhakikisha anatoka gerezani.

Wakili wa kujitegemea Michael Mwangasa, amesema wameshirikiana kuona kijana huyo anaachiwa huru kwa kulipa faini ya shilingi milioni 5 .

Naye Twaha Mwaipaya kwa niaba ya walioanzisha ukusanyaji fedha hizo kwa ajili ya kumsaidia kijana Chaula ameushukuru wananchi na wanaharakati kutoka maeneo tofauti hapa nchini kwa kuungana kuhakikisha kijana huyo anaepuka adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka miwili jela .

Baada ya hukumu hiyo wiki iliyopita kijana huyo alienda gerezani kuanza kutumikia kifungo cha miaka miwili jela na baadaye wanaharakati wakajitokeza kuanza kuchangisha mchango ili kupata fedha za kumtoa gerezani na kufanikiwa kupata zaidi ya sh.mil.6.

Jopo la mawakili na watu mbalimbali wamefika katika viunga vya magereza ya Ruanda jijini Mbeya ambapo baada ya kushughulikia mambo kadhaa kijana Shadrack Chaula ameachiwa na kwenda kuendelea na maisha yake ya kawaida.

Akisoma hati ya mashtaka leo Julai 4,2024 Mwendesha mashtaka wa serikali, Rosemary Mgeniji mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya wilaya ya Rungwe Mh. Ramla Shehaghilo ameeleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo 22/6/2024 katika kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Imeelezwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka kuwa mshtakiwa huyo akiwa dukani kwake maeneo ya Ntokela alirekodi ujumbe wa video wenye maneno“Kwakua umeshindwa kutetea taifa lako lisiathirike na ushoga hii video inakuhusu wewe na si mtu mwingine” ikiwa ni taarifa za uongo zenye kupotosha jamii.

Alipopewa nafasi ya kujitetea mahakamani hapo mtuhumiwa huyo Shadrack Chaula mkazi wa Ntokela amesema yupo tayari kutumikia adhabu yoyote atakayopewa na mahakama hiyo.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na mawakili wa serikali Veronica Mtafya na Rosemary Mgeniji umeiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine kwani kitendo hicho kimetafsiriwa kama udhalilishaji kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akitoa hukumu hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya wilaya ya Rungwe ,Ramla Shehaghilo amesema kwa mujibu wa sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha 16 amemtia hatiani kwenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya mil.5.

Hata hivyo mtuhumiwa amepelekwa gerezani kwenda kutumikia kifungo baada ya kushindwa kulipa faini ya sh.mil.5.