Na mwandishi wetu,timesmajira.
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk. Athumani Kihamia, amesema filamu ya Royal Tour inayotarajiwa kuzinduliwa kesho kutwa na Rais Samia Suluhu Hassan itasaidia kuongeza mapato ya nchi sio tu utalii pekee bali itakuwa katika nyanja zote ikiwemo sekta ya madini, kilimo, biashara na michezo.
Akizungumza na timesmajira kwa njia ya simu jana amesema kuongezeka kwa uchumi inatokana na watu wa mataifa mengi duniani kuifuatilia kwa karibu Tanzania kutokana na vivutio adimu vilivyopo nchini.
“Tanzania ina fursa katika nyanja mbalimbali na hivyo kupanua wigo wa ajira, kuongezeka kwa kipato na hata wanamichezo watajulikama zaidi na kupata fursa ya kwenda nje ya nchi kama wanamichezo wa kimataifa,” amesema
Ameongezea kuwa “Kwa sasa wananchi wengi wa mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani wamefurika mkoani hapa kujionea filamu hiyo ya kihistoria ya mkuu wa nchi mbunifu na mwenye upeo wa diplomasia ya kiuchumi,”amesema Dk. Kihamia.
Aidha, amesema wananchi wa mkoa wa Arusha wamefurahia uamuzi wa Rais Samia kuchagua kuzindua filamu hiyo ya kihistoria katika mkoa huu wenye utajiri mkubwa wa madini na utalii.
“Wafanyabiashara wanaojihusisha na shughuli za kuelekeza watalii, mahoteli, na biashara mbalimbali zikiwemo mbogamboga na matunda yanayosafirishwa nje ya nchi, wafugaji na hata wavuvi wameonekana wenye shauku ya kuona matunda hayo ya utalii unaotangazwa kwa weledi mkubwa chini ya uongozi wa Rais Samia,”amesema .
Dk. Kihamia amesema wao kama serikali ya mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na wadau na wananchi wamejipanga kuhakikisha kwamba juhudi hizo za Rais Samia na serikali yake zinaleta athari chanya kwa wananchi na wadau wa utalii kwa ujumla ukizingatia asilimia 80 ya mapato ya utalii wote nchini yanapatikana Arusha.
Dk. Kihamia amewaoma wananchi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo endelevu kwa haraka na kuwaombea viongozi wetu wakuu chini ya Rais Samia kuzidi kutatua changamoto mbalimbali kwa mujibu wa malengo na madhumuni yaliyopangwa na serikali ya awamu ya sita inalenga kuyafikia.
Amesema Mkoa wa Arusha licha ya kunufaika na utalii, umepiga hatua kubwa katika nyanja za elimu, afya, miundombinu ya barabara,maji na ujasiriamali.
“Tutazielekeza Halmashauri zetu kuchungulia kwa kina fursa hizi za utalii ili kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani kwa lengo la kuongeza uwezo wa kutoa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Arusha,”amesema.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi