January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Kigogo feki’ Jeshi la Polisi atiwa mbaroni

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mkazi mmoja wa Mkoa wa Simiyu, Maduhu Masanja maarufu kwa jina la Norbert Marcel (49) akituhumiwa kwa kosa la kujipatia kwa udanganyifu kiasi cha sh. 200,000 kutoka kwa mfanyabiashara mmoja wa mjini Shinyanga.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga, George Kyando amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kujifanya yeye ni Kamanda wa Upelelezi (RCO) mkoani Shinyanga, ambapo aliomba kiasi cha sh. 200,000 kutoka kwa mfanyabiashara, Hillal Soud ili aweke mafuta kwenye gari la polisi.

Kamanda Kyando amesema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kwa kosa la kufanya udanganyifu ni tukio la mara ya pili, ambapo awali Desemba 20, 2020 alikamatwa maeneo ya kituo cha zamani cha mabasi katika Manispaa ya Shinyanga alijifanya ni Kamanda wa kikosi cha Usalama barabarani mkoa (RTO) na kujipatia sh. 100,000 kinyume cha sheria.

Amesema kiasi hicho cha sh. 100,000 kiliombwa na mtuhumiwa kutoka kwa mwananchi mmoja aliyetambulika kwa jina la Hamisi Ally hata hivyo mtuhumiwa huo akiwa amefikishwa mahakamani mlalamikaji Hamisi aliandika barua Ofisi ya Mashitaka ya Taifa kanda ya Shinyanga akiomba kutoendelea na kesi hiyo ya jinai namba 5/2021 na mtuhumiwa aliachiwa huru.

Hata hivyo amesema inavyoonesha mtuhumiwa huyo amekuwa mzoefu katika kufanya vitendo hivyo ambapo ameendelea tena kutapeli watu kitendo ambacho ni kosa mtu kujifanya yeye ni askari polisi wakati siyo kweli.

“Mtuhumiwa huyu tunatarajia kumfikisha mahakamani hivi karibuni baada ya upelelezi kuhusu shauri lake kukamilika, inaonesha amekuwa na uzoefu wa kudanganya watu kwamba yeye ni polisi wakati siyo na kitendo hicho ni cha uhalifu na hufanya hivyo kwa lengo la kutaka kujipatia kipato,” ameeleza Kamanda Kyando.

Kamanda huyo wa Polisi ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa makini na watu wa namna hiyo na kwamba pindi watakapomuona mtu au kundi la watu wanaotaka kuwafanyia utapeli wasisite kutoa taarifa kwake kupitia namba yake ya simu namba 0739 009 957 ili watu hao waweze kukamatwa.