December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kigahe: Samia ameongeza kasi miradi ya uwekezaji

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

JUHUDI za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Serikali inaweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini zimezidi kuzaa matunda kutokana na kusajiliwa miradi mbalimbali zaidi 132 ya uwekezaji kuanzia Julai 2022/2023.

Miradi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 22 niikilinganisha kipindi cha mwaka 2021/22.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakati akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika mdahalo wa kiuchumi wa kujadili namna ya kuendelea kuboresha na kuvutia wawekezaji nchini hasa ikizingatiwa uwekezaji na ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza umezidi kuimarika.

“Haya ni matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia na hasa tukizingatia tunahitaji wawekezaji wote wa ndani na wa nje waweze kupata mazingira wezeshi,” alisema na kuongeza.

“Ongezeko hili limetokana na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini ambayo yameleta matokeo chanya kwenye sekta zote.”

“Haya ni matokeo ya mikutano ya huko nyuma ambayo tumekua tukijadiliana ili kuweka mazingira bora ya uwekezaji Tanzania,” alisema na kuongeza. “Hili limekua msisitizo wa Awamu ya Sita.”

Aidha Kigahe alisema kutokana na mazingira ya uwekezaji yalivyo mazuri, wanahakikisha wale ambao wamewekeza wanaendelea kunufaika na uwekezaji wao ndani.

Kuhusu sera ya viwanda na biashara, Kigahe alisema wanaendelea kuweka mikakati mahususi ya utekelezaji wa sera hizo, lakini pia kufanyia mapitio ili ziendane na hali halisi ya mahitaji ya sasa.

“Katika sekta zetu zote, sera ya biashara, viwanda, biashara ndogo na viwanda, sera hizi tunafanya mapitio ili ziendane na hali halisi ya mahitaji ya soko,” alisema.

“Tutaendelea kuweka mikakati mahususi ya utekelezaji wa sera hizo kwa sababu kuandika sera bila kuwa na mikakati mahususi kutekeleza sera hizo bado huwa ni changamoto”. Aliongeza Kigahe.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar alifurahi kushiriki hafla hiyo muhimu na kusena kwamba itasaidia kukuza uchumi wa Tanzania na kuleta uwekezaji bora .