Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetangaza mkakati mpya wa kuwabaini watumiaji wote wa dawa za kulevya nchini, ambapo hakuna mhusika yeyote atakayeachwa bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mkakati huo unatokana na mamlaka hiyo kununua mitambo ya kisasa ambayo tayari imewasili bandarini jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutumika kwenye maabara ya DCEA kwa ajili ya kupima na kubaini watumiaji dawa hizo.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, wakati akifunga semina ya siku mbili iliyoandaliwa na Mamlaka hiyo kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini.
Amesema Mamlaka hiyo inayo orodha ya watu wote wanaotajwa kutumia dawa za kulevya nchini, wakiwemo wasanii, hivyo baada ya mitambo hiyo kufungwa wote watapimwa.
“Tunayo orodha ya watu wote wanaotajwa kutumia dawa za kulevya, tutawapima na wale wote watakaobainika tutawachukulia hatua za kisheria,” amesema Lyimo na kuongeza;
“Kuna wasanii wanaohamasisha utumiaji wa dawa ya kulevye na tuna orodha ya wasanii wanaotumia dawa za kulevya na tunayo sheria ambapo kifungu 17 na 18 cha sheria hiyo kinatupa Mamlaka kumkamata mtu yoyote tunayemuhisi anatumia dawa za kulevya.”
Amesisitiza kuwa watawakamata na kuwapimwa kwani maabara ya kisasa inajengwa.
Amesema, maabara hiyo itakuwepo kwa ajili ya kuhakikisha wanatimiza sheria. “Watu wote tunaowahisi wanaotumia dawa za kulevya au wanahamasisha watu kutumia dawa za kulevya tutawakamata kupitia sheria hiyo, sheria inawaruhusu wakishapimwa na kubainika wanaotumia dawa za kulevya wanapelekwa mahakamani.
Mahakamani hukumu yao ni kifungo cha miaka mitatu gerezani, wakishafungwa miaka hiyo endapo kipimo kitadhibitisha kuwa yeye kaishakuwa mrahibu wa dawa, Hakimu atatoa hukumu nyingine kuwa apelekwe kifungo cha kupata tiba.
Kwenye sheria kifungu namba 31 kinaruhusu mtu akishahukumiwa pale kwa amri ya hakimu huyo mtu pamoja na kifungo alichotumikia, anatakiwa apate tiba kifungo hicho kinaruhusu kumtibu ya huyo mtu,” amesema Lyimo.
Amewataka watu wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kujirekebisha kwani mitambo ikikamilika wataanza kushughulika nao.
Akieleza madhara ya dawa za kulevya, amesema nchi yoyote duniani yenye matumizi makubwa ya dawa za kulevya, lazima uchumi wake utaathirika na nchi hiyo haiwezi kukua kiuchumi, kwa sababu kundi kubwa linalotumia dawa za kulevya ni vijana ambao ndio wenye nguvu, wazalishaji na watenda kazi.
“Hauwezi kukuta mzee wa miaka 70 anatumia dawa za kulevya, lakini kundi kubwa la wanaotumia dawa za kulevya ni kuanzia shule za msingi hadi vyuoni, hapo hapo ndipo kundi kubwa linapopotelea,” amesema.
Aidha, ametaja kundi lingine la wanaopotea kutokana na dawa za kulevya kuwa ni la wale ambao wako nje ya mfumo rasmi kuanzia miaka 10 na kuendelea hadi 30.
Amefafanua kwamba katika mazingira hayo nchi haiwezi kukua kiuchumi.
Ametoa mfano kwamba hivi sasa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, malengo yake makuu ni kuhakikisha inajenga uchumi endelevu.
“Uchumi endelevu ili uweze kufanikiwa kama kuna matumizi makubwa ya dawa za kulevya hatuwezi kufika mbali, kwa sababu ili kupata uchumi endelevu, lazima kuwe na uzalishaji endelevu, hivyo lazima upate kizazi endelevu kinachokua.
Lazima upate uogozi unaoridhisha wenye maono chanya, lakini mkiwa na viongozi ambao ni watumiaji wa dawa za kulevya hauwezi kuwa na uchumi endelevu, kwa sababu mwisho wa siku ukifanya maendeleo kidogo unaona ni makubwa kwa sababu ubongo wako hauna uwezo wa kufikilia mambo makubwa wala kuangalia mbele miaka 50 au 100 ijayo,”amesema Lyimo.
Amesema, hali ikiachwa hivyo tutakosa watu wa kuwa viongozi sahihi, mwisho wa siku tutakuta tunaongozwa kulingana na matakwa ya watu wengine na siyo kama tunavyotaka sisi.
“Kwa hiyo dawa za kulevya ni eneo ambalo linaweza kutumika kijasusi katika kuhakikisha kwamba linadidimiza uchumi wa nchi na linafanya watu wake waweze kutawaliwa kwa namna nyingine, hivyo tatizo hilo liangaliwe kwa jicho la kuona mbele zaidi,” amesema.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi