December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

????????????????????????????????????

Kesi ya wanandoa kujeruhi yaendelea kupigwa dana dana

Mtuhumiwa wa shambulio la kudhuru mwili, Bharat Nathwan (kulia) na mke wake, Sangita Bharat (kushoto) anayetuhumiwa kutoa matusi dhidi ya Lalit Ratilal wakiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kusikiliza kesi inayowakabili. 

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya tuhuma ya kujeruhi na kutoa lugha ya matusi  baada ya kudaiwa mahakamani hapo kuwa mke wa mshtakiwa Bharat Nathwan (57), Sangita Bharat (54)  ni mgonjwa hawezi kumsikiliza shahidi wa upande wa mashtaka.

Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania asili ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima – Kisutu, jingo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashtaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.

Taarifa hiyo imetolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya wa mahakama hiyo na Wakili wa washtakiwa hao, Edward Chuwa wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa shahidi watano wa upande wa mashtaka.

“Mheshimiwa tupo tayari kuendelea, kwa bahati mbaya tumepata habari mteja wangu Sangita ni mgonjwa anasumbuliwa na presha na nimonia,lakini alitamani kushiriki kwenye kesi, tunaomba akapumzike,”

“Tunaomba ahirisho ili mteja aende kupumzika nyumbani na pia tuna vyeti vya ugonjwa,”alidai Wakili Chuwa

Akijibu taarifa hiyo, Wakili wa Serikali Faraja Ngukah, alidai kuwa kuhusu suala la afya ya mtuhumiwa hawawezi kuipinga na kwa sababu wakili kadai ana vyeti basi vitolewe kama sheria inavyoelekeza.

“Kama anaumwa na wamekubalina na wakili wake haina shida, nimeona hivi vyeti vimeandikwa jina la Sangita na ndiyo mtuhumiwa, siwezi kusoma karatasi hizi nikasema anaumwa nini, tunaomba tarehe nyingine ya kusikilizwa,”alidai Wakili Ngukah

Baada ya Ngukah kudai hayo, Wakili Chuwa alipendekeza Septemba 26,2024 ndiyo kesi iendelee kusikilizwa, walikubaliana tarehe hiyo na mahakama ikaahirisha.

“Shahidi nakuonya ufike mahakamani Septemba 26,2024 kuja kutoa ushahidi mahakamani hapa, ufike bila kukosa,”alisema Hakimu Lyamuya

Ilidaiwa kuwa Nathwan Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jengo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.

Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwan peke yake, ambapo anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la Mrina-Kisutu ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiram Abdallah kwa kuzamisha kichwa chake kwenye chokaa.

Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwan peke yake, ambapo tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara Lalit Kanabar katika mwili wake kwa kumpiga ngumi na mateke kichwani.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi makubwa dhidi ya walalamikaji  kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.