Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mwanza
SERIKALI imeamua kutekeleza mradi wa shilingi bilioni 5.1 ili kuondokana na kero ya upatikanaji wa majisafi na salama inayowakabili wananchi wa Ilemela hususan Kata ya Buswelu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoani Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele wakati wa ziara iliyolenga kukagua ujenzi wa tenki la maji la lita milioni 3 linalojengwa kwenye kata hiyo.
Dkt. Lalika amesema, mradi huo wa tenki ni miongoni mwa miradi ambayo ilitengewa fedha Mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
“Serikali ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ilijipambanua vyema kutetea wananchi wake na kwamba mwananchi hapaswi kutembea zaidi ya mita 400 kufuatilia huduma ya maji,” amesema Dkt. Lalila.
Amesema, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mwananchi anapata muda mwingi wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo ili kujiongezea kipato na hivyo kukuza uchumi wake binafsi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa, anatambua miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na MWAUWASA kwenye wilaya hiyo na aliipongeza kwa jitihada zake katika kusimamia ujenzi wa miradi ya maji kwa niaba ya Serikali ambapo alisema kupitia miradi hiyo kero ya maji inakwenda kuwa historia.
“Natambua MWAUWASA inatekeleza miradi mingine ya maji Wilayani Ilemela mbali na huu tuliotembelea leo ambayo ni pamoja na Mjimwema, Nyasaka, Nyamhongolo, Kabusungu, Kabangaja, Igalagala na Kayenze, ninaamini kero ya maji itabaki historia,” amesema Dkt. Lalika.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Mhandisi Msenyele amesema unagharamiwa na Serikali kwa asilimia Miamoja kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa wahisani ambao ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa ambapo ujenzi wa tenki hilo ulianza rasmi Septemba, 2020 na kwamba unatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Julai 2021.
“Shughuli tunazoendelea nazo hivi sasa ni kuandaa umwagaji wa zege ya awali ya kuandaa kitako cha tanki, kutengeneza barabara ya kuelekea kwenye tenki pamoja na maandalizi ya umwagaji zege za kuta za tenki,” amesema Mhandisi Msenyele.
Mradi unahusisha ujenzi wa tenki la lita milioni tatu, ulazaji wa bomba urefu wa kilomita 14 na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji kufika kwenye tenki ambacho kinajengwa kwenye eneo la Kiseke Jeshini.
Amebainisha kuwa, kukamilika kwa mradi huo wa tenki kutanufaisha wananchi wa maeneo ya Buswelu, Lukobe, Kigala, Nsumba, Kahama, Bujigwa, Nyamadoke na Ilalila.
Mhandisi Msenyele amesema, mradi huo ni sehemu ya Programu ya Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mwanza (LV WATSAN) na kwamba unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba