Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online Mwanza
Kaya 106 kutoka Kata mbili za Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, zimepatiwa mbuzi 424,wenye thamani ya kiasi cha milioni 36.04,huku zikitakiwa kuhakikisha wanatunza Mifugo hiyo ili iweze kuzaliana na kuwasaidia kiuchumi.
Kaya hizo ni kutoka Kata ya Sangabuye na Nyamh’ongolo,ambao ni wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini(TASAF) kupitia mradi wa kuongeza kipato unaofadhiliwa na OPEC.
Ambapo Mtaa wa Igalagala uliopo Kata ya Sangabuye wamepata mbuzi 196 na mtaa wa Ibinza Kata ya Nyamh’ongolo wamepatiwa mbuzi 228 ambapo kila kaya imepatiwa mbuzi wanne kati yao watatu ni majike na mmoja ni dume .
Akizungumza wakati wa kuwakabidhi mbuzi hao kwa kaya hizo,Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ilemela Leonard Robert, ameeleza kuwa waanayo matarajio makubwa kuwa uchumi wa kaya hizo unaenda kuimarika kupitia mradi huo.
Hivyo amewataka walengwa wa TASAF kuupokea mradi huo kwa mikono miwili na kuhakikisha wanawatunza mbuzi hao ili waweze kuzaliana na baadae waje kuwasaidia katika utatuzi wa changamoto za kiuchumi katika kaya zao ikiwa ndio lengo la mradi huo.
Ameeleza kuwa wanaamini mradi huo unaenda kutatua changamoto za kiuchumi ndani ya familia hizo.
“Uchumi wa kaya unaenda kuimarika na changamoto zinaenda kupungua ambapo kila kaya itakuwa na jukumu la kuwatunza na kuwalinda, “ameeleza Leonard.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo Leah Mabula,ameishukuru Serikali chini ya kwa kutoa fedha hizo na kuahidi kutunza mbuzi hao waweze kuzaliana ili familia yake iweze kujikomboa kiuchumi
Diwani wa Kata ya Nyamh’ongolo,Andrea Nginila ameeleza kuwa mradi huo utaenda kuleta tija kwa wananchi wake kwa kuwaondolea umasikini hivyo kuwazalishia fedha za kujikimu wao binafsi na wategemezi wao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Suzana Tilumanywa amewataka wanufaika pamoja na uongozi wa kata na mtaa kuhakikisha wanaulinda mradi huo na kuutunza ili tija iliyokusudiwa iweze kufikiwa.
Huku akitoa ushauri kwa wataalam wa wilaya wakiwemo maofisa mifugo kufuatilia changamoto za walengwa hao na kuzipatia ufumbuzi na kueleza kuwa Ilemela imekuwa ya kwanza kutekeleza mradi huo hivyo wakifanya vizuri na wenzao wa maeneo mengine watakuja kujifunza kutoka kwao.
More Stories
Mhagama atoa somo kwa watendaji
Ilemela nyama choma festival, yazinduliwaÂ
Mchengerwa:Rufaa 5,589 za wagombea zimekubaliwa