Na Bakari Lulela,TimesMajira Online, Dar
KATIBU Mkuu UVCCM Taifa Kenani Kihongosi amewataka Vijana nchini kuwa wazalendo kwa taifa, pamoja na kutunza tunu ya amani na utulivu ili kuchochea maendeleo kwa Taifa.
Wito huo ameutoa wakati akifanya mahojiano na mtandao huu wakati wa zoezi la kusikiliza ushauri,maoni na changamoto kutoka kwa vijana wa kada mbalimbali katika ofisi za Uvccm zilizopo upanga jijini Dar es salaam.
Kihongosi amesema kwamba vijana wanapaswa kuwa wazalendo na taifa lao kwa kufanya kazi kwa nidhamu na maadili mema katika utumishi wao pindi wanapoaminiwa na kuteuliwa kushika nafasi za uongozi.
“Vijana wafanye kazi vizuri ili waendelee kuaminiwa,sisi tuliopewa nafasi za uongozi tuhakikishe tunazitumikia vizuri ili vijana tuendelee kuaminiwa katika teuzi zinazokuja,kwahiyo tuendelee kufanya kazi kwa bidii ili tuwe mfano kwa vijana wengine waliopo nyuma yetu ” amesema Kihongosi.
Katika hatua nyingine Katibu huyo Mkuu Taifa wa Uvccm aliwaomba wananchi kuendelea kujitokeza kwa hiari kupata chanjo ya ugonjwa wa uviko 19 huku akiwasihi kuacha kusikiliza taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa.
” Tunawajibu wa kuhakikisha tunachukua tahadhari , tupate chanjo kwa hiari hivyo wanaopata fursa ya kuchanja wachanje kwa mustakabali wa kulinda afya yao” alisema Kiongozi huyo.
Kuhusu Changamoto zinazowakabili vijana Kihongosi alisema vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira na mitaji licha yakua na elimu ambapo wengi wao wameshindwa kuwekeza taaluma zao katika kujiajiri.
Changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi hapa nchini ni kukosa nafasi za ajira na mitaji wanapomaliza masomo yao, lakini najaribu kushauriana nao kuona wanaweza kuwekeza vipi elimu yao katika kujiajiri na kujikwamua kiuchumi” alisema na kuongeza kwamba
Zoezi la kusikiliza maoni , ushauri na changamoto za vijana litakua likifanyika mara moja kila mwezi ambapo amewaomba vijana kuendelea kujitokeza kutoa maoni na ushauri kwa ajili ya kuleta ufanisi katika Jumuiya ya Uvccm pamoja na kujadili namna ya kutatua changamoto zinazowakabili vijana.
Kenani Kihongosi aliwahi kuwa mwenyekiti Uvccm mkoa wa Iringa, Mkimbiza Mwenge wa uhuru, na baadae aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Arusha kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu