March 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu Nishati aipongeza Sweden kufadhili miradi ya umeme nchini

  • Ni nchi ya kwanza kufadhili miradi ya umeme vijijini nchini
  • Ufadhili wake Mradi wa Makambako- Songea wawezesha vijiji 120 kupata umeme
  • Balozi wa Sweden nchini atoa pongezi kwa TANESCO na REA usimamizi wa miradi ya umeme

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba ameipongeza Serikali ya Sweden kwa kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya umeme ikiwa ni pamoja na mradi wa Makambako hadi Songea.

Pongezi hizo zimetolewa Februari 27, 2025 jijini Dodoma, wakati wa hafla ya kufunga rasmi Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme kutoka Makambako hadi Songea, uliofadhiliwa na Serikali ya Sweden kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Mhandisi Mramba amesema, mradi huo wa njia ya umeme kutoka Makambako hadi Songea umehusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye msongo wa kilovoti 220 kwa urefu wa kilomita 245, ujenzi wa vituo vya umeme vya Madaba na Songea mjini, upanuzi wa kituo cha umeme cha Makambako pamoja na kusambaza umeme katika vijiji 120.

“Tunaipongeza Serikali ya Sweden kwa mchango mkubwa ambao wanatusaidia katika kufadhili miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo kupeleka umeme vijijini hapa nchini,” amesema Mramba.

Amesema, Serikali ya Sweden imetoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini iliyotekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya za Urambo, Serengeti, Simanjiro na Ukerewe, pia Sweden ndio nchi ya kwanza kusaidia miradi ya umeme vijijini hapa nchini.

Miradi mingine iliyofadhiliwa na Sweden ni mradi wa ujenzi wa Bwawa la Mtera na Kidatu.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Sweden kwa sasa inaendeleza ukarabati wa kituo cha kuzalisha umeme cha Hale ambacho ni cha muda mrefu ambacho kitazalisha megawati 21 baada ya ukarabati kukamilika.

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya umeme.

Amesema mradi wa Makambako hadi Songea uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka 20 kukamilika kwake kutaendelea kunufaisha wananchi wengi katika upatikanaji wa huduma ya umeme hasa maeneo ya vijijini.